Back to top

Ajira za watu zaidi ya 500 katika Sekta ya Madini ziko mashakani.

25 May 2018
Share

Ajira za watu zaidi ya 500 katika sekta ya madini ziko mashakani kupotea kufuatia wamiliki wa viwanda 25 vya kuchenjua na kununua dhahabu vilivyoko mkoani Mwanza kutishia kuvifunga, baada ya Mkuu wa mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel kuzuia usafirishaji wa malighafi inayotumika kubebea dhahabu maarufu kama Carbon kutoka Geita kwenda Mwanza mahali vilipo viwanda hivyo.

Wachenjuaji na wanunuzi hao wa dhahabu wamesema hawako tayari kwenda kuwekeza mkoani Geita ambako hakuna soko la dhahabu na pia kwa kuhofia usalama wa mitaji yao kwani uwekezaji waliokwisha ufanya katika mkoa wa Mwanza ni mkubwa unaofikia zaidi ya shilingi Bilioni 15 za Kitanzania.

Kamishna Msaidizi wa madini Kanda ya Ziwa Victoria Magharibi Yahya Semamba naye ameunga mkono agizo la Mkuu wa mkoa wa Geita la kutosafirisha Carbon kwenye viwanda vya uchenjuaji mkoani Mwanza.

Mkuu wa mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel Aprili 24 mwaka huu alipiga marufuku usafirishaji wa Carbon za mkoa wa Geita kwenda Mwanza kwa ajili ya uchenjuaji wa dhahabu akidai zinaupotezea mkoa wake asilimia 60 ya mapato ya thamani ya dhahabu inayochimbwa mkoani humo.