
Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi Tanzania (CRB), Mhandisi Rhoben Nkori, amewaonya wataalamu kutokubali kutumika na kampuni za kigeni katika usajili wa ukandarasi ili kampuni hizo zionekane za kizawa (Local Contractors).
Amesema wapo baadhi ya wataalamu ambao huthubutu kudanganya wanahisa kati ya asilimia 51 ili kampuni zibadilishwe na kuwa za kizawa wakati wakijua wameahidiwa mishahara peke yake.
Nkori amesema hayo leo wakati akifungua mafunzo ya Usimamizi wa Fedha kwa Makandarasi kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini yanayo fanyika kwa siku tatu Mkoani Iringa.
Amesema kufanya hivyo ni kosa kisheria na kwamba atakaye bainika atafutiwa kampuni iliyosajiliwa na kufungiwa ili asisajili kampuni nyingine ndani ya miaka mitatu.
"Hakuna anaye kuzuia kama muungano wenu ni wa kibiashara. Unapewa hisa ubadilishe kampuni iwe ya kizawa unakubali wakati unajua unachpata ni mshahara peke yake," amesema na kuongeza;
"Unachofanya ni kuidhulumu nafasi yako, unawadhulumu watanzania wenzako na unaidhulumu nchi yako, unakuwa mbele ili kampuni iwe ya kizawa wakati sio ya kizawa."
Aidha Msajili huyo wa CRB amewatoa hofu kuwa kinacho zungumzwa na Serikali kuhusu makandarasi wazawa kupewa kipaumbele kwenye kazi ni kweli.
"Kila mmoja amesikia jitihada za Serikali jinsi ya kuwezesha makandarasi wazawa sio siasa, ni kweli na sisi tulio ndani tunaona," amesema na kuongeza;
"Cha msingi watakao bahatika kufanya kazi kwa awali wawe waaminifu kuiaminisha Serikali kwamba makandarasi wa ndani tunaweza na hiyo itaongeza imani kwa Serikali na baadae fedha zinazo enda kwa makandarasi wa nje, zitakuja ndani," amesisitiza.
Awali Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (CRB), Nisile Mwandetele amesema mafunzo hayo ni muhimu na yanalenga kuimarisha kazi ya ukandarasi.
Amewataka wakandarasi hao kuwa waaminifu wakati wanapopewa kazi.
Kwa upande wao baadhi ya wakandarasi walisema mafunzo hayo ambayo huwa yanatolewa mara kwa mara yamekuwa yakiwaimarisha katika utendaji wao tofauti na kama yasingekuwepo.
"Binafsi mafunzo yamekuwa muhimu sana kwangu na sijawahi kukosa tangu niwe mkandarasi," amesema Vitus Mushi, mmoja wa wakandarasi.
