
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na wananchi na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama, imewakamata watu sita wakiwa na kilo mia tatu arobaini na mbili za bangi.
Aidha, limekamata kilo mia moja na mbili za mbegu za zao hilo na kuteketeza ekari elfu moja mia moja sitini na tano za zao hilo, katika operesheni maalum wilayani Kilosa mkoani Morogoro.
Akizungumza mara baada ya utekelezaji wa mashamba hayo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo, amesema mashamba ya bangi yaliyoteketezwa yamelimwa pembezoni mwa mto Mbakana, Misigiri na Mgeta kwenye eneo la akiba la hifadhi ya Taifa Mikumi.
Amesema uharibifu mkubwa wa mazingira umefanyika katika eneo hilo ambalo miti imekatwa ili kupata eneo la kulima bangi, kuharibu uoto wa asili.
Kadhalika, amewashukuru wananchi hususan vijana waliojitolea kushiriki katika zoezi la utekelezaji wa mashamba ya bangi pamoja na serikali kwa kuiwezesha mamlaka kufanya operesheni za kuteketeza mashamba ya bangi na kutokomeza dawa za kulevya nchini Tanzania.
