Back to top

FICHUENI TAASISI ZA UKOPESHAJI ZISIZO RASMI.

24 May 2024
Share

Wananchi wametakiwa kushirikiana na Viongozi wa Serikali kuwafichua wamiliki wa Taasisi za Ukopeshaji fedha  zisizo rasmi ambazo zinajali zaidi maslahi yao binafsi, ili watakaobainika  hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, Bw. John Wanga, alipokutana na Timu ya wataalamu ya Wizara ya Fedha ambao wanaendelea kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa mkoa wa Kagera .

Alisema kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua watu wote watakaobainika kwenda kinyume na maelekezo waliyopewa na Benki Kuu ya Tanzania kabla hawajapatiwa leseni ya kuendesha shughuli za utoaji mikopo.

Naye Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bi.Mary Mihigo, aliwasisitiza wananchi kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha na kutunza akiba.

Wizara ya Fedha inaendelea na zoezi la utoaji elimu kwa wananchi kuhusu huduma ndogo za fedha ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na elimu ya huduma ndogo za fedha.