Back to top

Jamii yatakiwa kutoa ushahidi juu ya ukatili wa kijinsia Rukwa.

21 June 2019
Share

Viongozi wa dini mkoani Rukwa wameitaka jamii kubadilika na kuanza kutoa ushirikiano wa dhati, katika kutoa taarifa juu ya vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto, ikiwa ni pamoja na mimba kwa wanafunzi wa kike, na kisha kushiriki kikamilifu katika utoaji ushahidi kwenye vyombo vya sheria kuliko ilivyo hivi sasa.
 
Wakizungumza mjini Sumbawanga mkoani Rukwa, juu ya vitendo vya kikatili vilivyokithiri mno mkoani humo, vinavyochangia kwa kiasi kikubwa mimba za utotoni, na idadi kubwa ya watoto kwenda kuishi katika mazingira hatarishi maarufu kama watoto wa mitaani, wamesema mashauri mengi ya ukatili yanaripotiwa kwenye vituo vya polisi, lakini yanashindwa kufikishwa mahakamani kwa kukosa ushahidi jambo ambalo linafanya vita dhidi ya vitendo hivyo kuwa ngumu mno.
 
Kwa upande wake katibu tawala wa mkoa wa Rukwa Bw.Mernad Makali, akizungumza mjini Sumbawanga na wadau juu ya mkakati shirikishi wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto, amesema katika kipindi cha 2017 hadi mwaka uliopita wa 2018 wanafunzi wa kike 149 walipata ujauzito, 59 miongoni mwao wakiwa ni wanafunzi wa shule za msingi, na huku matukio ya kikatili zaidi ya 4,600 yakiripotiwa kwenye vituo vya polisi.