Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Charles Mbuge amezindua Ghala katika kikosi cha Jeshi hilo 847 Milundikwa wilayani Nkasi mkoani Rukwa lililojengwa na Vijana wa JKT Operesheni Makao Makuu kwa Garama za Shilingi Milion 179 lenye ukubwa wa kuhifadhi Tani 2000 ambapo kwa sasa lina Tani 1000 za Mazao.
Ametoa kauli hiyo katika Kikosi cha 847 KJ cha Milundikwa wilayani Nkasi Mkoani Rukwa alipokuwa akieleza kilimo cha kimkakati kinachotekelezwa na jeshi hilo.
Ameeleza kuwa ifikapo mwaka 2024/25 jeshi hilo litakuwa na uwezo wa kulima ekari 28,000 za mazao mbalimbali kwenye vikosi vyake ili kujitosheleza kwa chakula.
Amesema kutokana na mikakati iliyowekwa kwenye kilimo ndani ya jeshi hilo ifikapo mwaka huo watakuwa na uwezo wa kulima hekari hizo ambapo kwa sasa katika msimu wa kilimo wa mwaka 2020/21 Ekari 12,247 za mazao mbalimbali ikiwamo mpunga na mahindi zimelimwa.
Amebainisha malengo ya JKT ifikapo mwaka huo wajitegemee kwa chakula kwa asilimia 100, ili kuipunguzia serikali gharama za kuwahudumia vijana wa JKT na badala yake fedha hizo zitumike kwenye ujenzi wa miundiombinu ya elimu na afya.
"Tunataka ifikapo mwaka 2024/25 tuwe na uwezo wa kulima ekari 28,000 ambazo zitakuwa tayari zinajitosheleza kujilisha ndani ya JKT, na jamii yetu inanufaika kwa mambo mengi kwa mfano Chita kuna maji yalikuwa yanatoka milimani na kuathiri mashamba tumedhibiti kwa kujenga skimu za umwagiliaji na wananchi wameondokana na mafuriko ya mara kwa mara"Amesema Mbuge.
Amesema uzalishaji huo utakapojitosheleza ndani ya jeshi na kuwa na ziada itauzwa kwa wananchi ili jeshi lipate faida zaidi.
Mkuu huyo amesema wataendelea kujenga maghala hayo maeneo mbalimbali wanayolima maharage na mahindi.
Awali, amefafanua maono ya jeshi hilo kujitegemea kwa chakula kuwa ni alipoteuliwa na Rais Dk.John Magufuli walikaa na wenzake na kuangalia sekta ambayo itasaidia JKT kusonga mbele na kuona ni sekta ya kilimo.
"Niliunda kamati na tulianza na kilimo cha dharura kwa mwaka 2019/20 katika vikosi viwili ndani ya JKT tukalima ekari 2200, lakini ndani ya JKT kwa ujumla tulilima ekari 8,517, mikakati iliyokuwepo katika kikosi chetu cha Chita 837 KJ Morogoro tulilima hekari 1000 za mpunga, na kikosi cha Milundikwa 847 KJ tulilima mahindi hekari 1000 na maharage hekari 200,"Amesema Mbuge