Back to top

Magufuli amtumbua Kichere TRA na Kakunda Kilimo Kisha kuteua tena.

08 June 2019
Share

Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt.John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bwana Charles Edward Kichere na kumteua Bw. Edwin Mhede kuchukua nafasi hiyo.

Kwa Mujibu wa Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, IKULU imeeleza kuwa aliyekuwa Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Charles Edward Kichere ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Erick Shitindi ambaye amestaafu. 

Kamishna mpya wa TRA Bwana.Mhende aliyechukua nafasi ya Bwana Kichere, kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara.

Pia Rais Magufuli amteua Mhe.Innocent Lugha Bashungwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, na kisha kutengua uteuzi wa Mhe.Joseph George Kakunda ambaye uteuzi wake umeutengua, ambapo kabla ya uteuzi huo, Mhe. Bashungwa alikuwa Naibu Waziri wa Kilimo.

Taarifa hiyo ya Ikulu imeongeza kwa kueleza kuwa Uteuzi wa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara utafanywa hapo baadaye, sababu za kutenguliwa hazikuwekwa bayana.

Itakumbukwa tu kwamba siku ya Juni 7, 2019, Rais Dkt.John Pombe Magufuli alikuwa na kikao na Wafanyabiashara ambapo walieleza yale yanayowasibu mbele ya Rais Magufuli Ikulu Dar es Salaam.

Hata hivyo miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa ndani ya kikao cha wafanya biashara na Rais ni pamoja na kutoa majibu kuhusu maoni na changamoto mbalimbali za wafanyabiashara zikiwemo zinazohusu uboreshaji wa mazingira ya biashara na uwekezaji, uwingi wa taasisi za kudhibiti biashara na uwekezaji ambazo zimekuwa zikikwamisha shughuli hizo na kufungwa biashara.

Changamoto nyingine ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoza kodi kubwa ikilinganishwa na biashara inayotozwa, ukusanyaji wa kodi kwa vitisho, vitendo vya rushwa, unyanyasaji wa wafanyabiashara na wawekezaji na kuwepo kwa tozo zenye kero ambazo hukwamisha maendeleo ya biashara na uwekezaji na kuvutia ukwepaji wa kodi na vitendo vya rushwa, hali inayoonekana kupelekea Rais Magufuli kutengua uteuzi wa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bwana Charles Edward Kichere na kisha kumteua Bw. Edwin Mhede kuchukua nafasi hiyo.

Mhe.Rais Magufuli alitumia nafasi hiyo kukemea vitendo vya watumishi wa umma waliopo katika mamlaka za udhibiti na ukusanyaji wa kodi na tozo mbalimbali kuacha kuwanyanyasa wafanyabiashara na pia amewataka wafanyabiashara hao kuacha kukwepa kodi, kutoa rushwa na kufanya udanganyifu katika biashara zao.

“Ndugu wafanyabiashara nataka muitangulize Tanzania mbele, tunahitaji kodi lakini sio kodi ya unyanyasaji, sipendi kuona mfanyakazi wa TRA anamnyanyasa mfanyabiashara, na sipendi mfanyabiashara anamnyanyasa mfanyakazi wa TRA” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Kufuatia changamoto mbalimbali zilizoibuliwa jana na wafanyabiashara katika mkutano huo, Mhe. Rais Magufuli alichukua hatua za papo hapo zikiwemo kuagiza Afisa Upelelezi wa Mkoa wa Morogoro (RCO) SSP. Asifiwe Ulime kusimamishwa kazi na kuchunguzwa kufuatia unyanyasaji uliofanywa na Polisi dhidi ya watumishi wa kiwanda cha tumbaku (TLTC), kuchunguzwa na kuvuliwa madaraka kwa Meneja wa TRA Mkoa wa kikodi wa Ilala Jijini Dar es Salaam Bw.Abdul Mapembe kufuatia kufungwa kampuni ya kazi za sanaa ya Steps Entertainment bila sababu za msingi na kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa maafisa 3 wa TRA ambao walizuia mzigo wa mfanyabiashara mmoja kwa miaka 3 huku wakishinikiza kupewa rushwa.

Kwa upande wa Wizara ya Kilimo nayo iliguswa kwenye mkutano huo ambapo pia ilitupiwa lawama katika utendaji kazi wake, licha ya wafanya biashara kuzungumza mengi Mwanasiasa mkongwe nchini, Dkt.Chrisant Mzindakaya alieleza mbele ya rais na kusema kwamba tangu Tanzania ipate uhuru mwaka 1961, Wizara ya Kilimo imekuwa ikiliangusha Taifa.

 Mzindakaya Alisema “Kilimo ni sayansi sio hotuba tena kitaalamu, taasisi zote za kilimo katika wizara hii zinakufa na ushahidi ni Uyole-Mbeya ilikuwa inawika leo ni taabani sasa kilimo kitaendeleaje?, alihoji kwenye Mkutano wa Wafanyabiashara Ikulu Dar es Salaam jana.

Aliendelea kueleza anachokiona huku akieleza kwa hisia mbele ya Rais pamoja na wafanyabishara kwamba “Huyu waziri wako wa Kilimo aamke nipo tayari kumshauri na hawa vijana wako wakubali wazee tuwape ushauri naweza kusaidia bado, wala siombi kazi kwa mtu mimi, nitasaidia maana ninapenda unavyoendesha nchi,”alisema Dk. Mzindakaya.

Kama tujuavyo Rais Magufuli huwa si mwenye kupepesa macho inaonyesha wazi kutengua uteuzi wa Mhe.Joseph George Kakunda ambaye alikuwa Waziri wa Viwanda na Kumteua Mhe.Innocent Lugha Bashungwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara ni kutokana na malalamiko yaliyoelekezwa kwenye wizara hiyo wakati wa mkutano wa wafanyabiashara na Rais Ikulu Dar es Salaam.

Kwenye mkutano wa jana Juni 07, 2019, ulihudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe.Prof. Adelardus Kilangi, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wabunge, Wakuu wa Taasisi mbalimbali za Serikali, Chama cha Wenye Mabenki Tanzania na wafanyabiashara 5 kutoka kila Wilaya hapa nchini.