Back to top

Majeshi ya polisi Kusini mwa Afrika kufanya operesheni za pamoja.

08 June 2019
Share

Wakuu wa Majeshi ya Polisi Kusini Mwa Afrika (SADC), wamekubalina kufanya operesheni za pamoja zitakazowezesha kupambana na matukio mbalimbali ya kihalifu ikiwemo matukio ya wizi wa magari, uuzaji wa dawa za kulevya pamoja na kupambana na biashara ya usafirishaji wa binadamu na uhalifu unaovuka mipaka.

Akizungumza baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere JNIA akitokea nchini Zambia, ambapo alihudhuria mkutano wa Wakuu wa polisi Kusini Mwa Afrika na Wakuu wa Upelezi, IGP Sirro amesema kuwa, majeshi wanachama wa SADC wamekubaliana katika kubadilishana taarifa za uhalifu na wahalifu hatua ambayo itasaidia katika kubaini viashiria vya kigaidi.

IGP Sirro amesema kuwa, miongoni mwa mambo ambayo yalipewa kipaumbele katika mkutano huo uliofanyika mjini Lusaca, ni pamoja na uhalifu kwa njia ya kimtandao ambapo watu wasiokuwa waaminifu ukimbilia kufanya uhalifu kwa kutumia njia hiyo ambapo kwa pamoja wamekubaliana kuendelea kudhibiti vitendo hivyo.

Aidha, IGP Sirro amezungumzia hali ya usalama nchini hususan katika kipindi cha sikukuu ya Eid El Fitr ni kwamba hakuna matukio ya uhalifu yaliyoripotiwa kama uhalifu wa kutumia silaha za moto, wizi wa watoto na matukio mengine ambayo yanalenga jamii.

Naye Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI Robert Boaz, amesema kuwa, nchi nyingi Barani Afrika zimekuwa na makubaliano ya pamoja hususan katika kujenga ushirikiano baina ya majeshi na Jeshi ili kuwabaini wahalifu wanaokimbilia nchi nyingine hatua ambayo itasaidia kubaini na kutambua uhalifu na wahalifu.