Back to top

Mugabe kuzikwa makaburi ya kitaifa ya mashujaa mwezi ujao.

14 September 2019
Share

Mwili wa Rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Gabriel Mugabe utazikwa mwezi ujao.

Hayo yametangazwa na Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa, aliyeongeza kuwa marehemu atazikwa katika makaburi ya kitaifa ya mashujaa, baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kaburi lake.

Awali kulikuwa na mvutano kati ya familia ya Mugabe na serikali kuhusu ni wapi kiongozi huyo aliyeiongoza Zimbabwe kwa miaka 37 anapaswa kuzikwa kwa heshima zote za kitaifa.

Hafla rasmi ya kumuaga Mugabe imepangwa kufanyika katika uwanja wa taifa mjini Harare, ambapo viongozi kadhaa wa Afrika pamoja na marais wa zamani wanatarajiwa kuhudhuria.

Siku ya jumapili mwili wa rais mstaafu Mugabe utasafirishwa hadi kijijini kwao Zvimba, kwa tambiko za kitamaduni na pia mazishi ya ishara kabla ya maziko kamili mwezi ujao.

Rais mstaafu Mugabe alifariki Dunia Singapore wiki iliyopita akiwa na umri wa miaka 95, na mwili wake ulirudishwa Zimbabwe siku ya Jumatano.