Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu amewataka wananchi wenye leseni za kuchimba madini ndani ya Hifadhi za Misitu, mapori ya Akiba pamoja na Hifadhi za Taifa wafuate sheria zinazotakiwa kabla ya kuanza kazi ya machimbo.
Amewaeleza wananchi hao licha ya kuwa wana leseni inayowaruhusu kuchimba madini ndani ya Hifadhi wanachotakiwa ni kuomba vibali kutoka kwenye Taasisi husika za Uhifadhi.
Mhe.Kanyasu amefafanua kuwa kuingia ndani ya Hifadhi na kuanza kuchimba madini bila kuwa na vibali kutoka kwa Taasisi husika ya uhifadhi ni kosa kisheria na endapo watakutwa watakamatwa na sheria itafuata mkondo wako
Ametoa msimamo huo jana mkoani leo Geita wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wakazi wa eneo la Mgusu ambao shughuli yao kuu ya kiuchumi ni Uchimbaji wa madini ya Dhahabu.
Kufuatia hali hiyo Mhe.Kanyasu amewataka Wananchi wenye leseni za kuchimba madini ndani ya Hifadhi ya msitu unaosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania
(TFS) katika eneo hilo la Mgusu waombe kibali kutoka TFS ili waendelee na shughuli za machimbo bila kubugudhiwa.
Amesema kumekuwa na mazoea kwa wananchi mwenye leseni za kuchimba madini ndani ya Hifadhi kufikiri kuwa Kwa vile wana leseni hiyo basi wana haki ya kuanza kuchimba madini bila ya kuwa na kibali kutoka TFS.
Kanyasu amewaeleza wananchi hao kuwa inapotokea ardhi ina madini kunakuwa na umiliki wa aina mbili, kunakuwa na umiliki wa leseni ya juu ya ardhi na leseni ya chini ya ardhi, hivyo mwenye leseni ya chini ya ardhi akitaka kuchimba madini chini ya ardhi anatakiwa aombe kibali kwa mwenye leseni ya juu ya ardhi ambapo katika eneo hilo wenye ardhi ya juu ni TFS.
Hivyo amewataka wananchi hao kama wanataka kuanza kuchimba madini ndani ya msitu huo waombe kibali kutoka TFS kwa sababu kwa mujibu wa sheria TFS ndio yenye leseni ya umiliki wa juu ya ardhi.
Amesema wakikubaliana na TFS watapewa utaratibu wa kulipa kiasi fulani cha pesa pamoja kuonesha mpango wa kurudishia miti mara baada ya shughuli za uchimbaji madini utakapomalizika
Aidha, Mhe. Kanyasu amewataka wananchi wa eneo hilo waache tabia ya kukata miti kwa ajili ya shughuli za madini pasipo kuomba kibali kutoka TFS
''Tutakayemkamata akifanya uharibifu ndani ya Hifadhi ya misitu huo, tutahakikisha analipa gharama zote za miti atakayokamatwa nayo'' alisisitiza Mhe. Kanyasu.