Back to top

NEC yatangaza tarehe ya kufanyika kwa Uchaguzi Mdogo wa Udiwani.

22 May 2019
Share

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza tarehe 15, Juni mwaka huu kuwa ni siku ya kufanyika kwa Uchaguzi Mdogo wa Udiwani katika kata 32 zilizopo katika halmashauri ishirini (20) za Tanzania Bara.

Akizungumza ofisini kwake jijini Dar es Salaam Makamu, Mwenyekiti wa NEC Jaji (R) Mbarouk S. Mbarouk amesema kuwa, Tume imetangaza tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi huo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya serikali za Mitaa, juu ya uwepo wazi wa nafasi 31 za Udiwani katika Kata 31 za Tanzania Bara kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kujiuzulu na vifo.

Aidha, amesema kuwa, Tume imetangaza kufanyika kwa Uchaguzi Mdogo wa Udiwani katika kata ya Kitangiri Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela jijini Mwanza sambamba na kata hizo 31, baada ya Mahakama ya Rufaa kuondoa maombi ya mapitio yaliyowasilishwa katika Mahakama hiyo, kufuatia kutenguliwa kwa matokeo ya Uchaguzi wa Udiwani katika kata hiyo.

Jaji (R) Mbarouk amesema kuwa, fomu za uteuzi wa Wagombea zitatolewa kati ya tarehe 27 hadi 31 Mei, uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 31 Mei, kampeni za uchaguzi zitaanza tarehe 01 Juni hadi 14 Juni mwaka huu na tarehe 15 Juni, mwaka huu ndiyo itakuwa siku ya uchaguzi.

Aidha Tume ya Taifa ya Uchaguzi imevikumbusha vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni, maadili ya Uchaguzi, taratibu, miongozo na maelekezo yanayotolewa na Tume wakati wote wa kipindi cha Uchaguzi huu mdogo.

Wakati huo huo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imefanya uteuzi wa Madiwani Wanawake wa Viti Maalum saba (07) katika Hamlashauri za Manispaa za Sumbawanga na Tunduma, Halmashauri za Wilaya za Tandahimba, Korogwe na Rombo.