Back to top

Nyama zisizofaa zakamatwa zikiuzwa kwa wananchi Arusha.

07 June 2019
Share

Wakaguzi wa nyama mkoa wa Arusha wakishirikiana  na watendaji wa bodi ya taifa ya nyama wamekamata nyama zisizofaa kwa matumizi ya binadamu zikiuzwa kwa wananchi.

Nyama hizo zinazokadiriwa kuwa na kilo zaidi ya 400 zimekamatwa katika operesheni inayoendelea ya kukagua mabucha ya nyama katika maeneo mbalimbali suala ambalo kaimu msajili wa bodi ya nyama Bw Imani Sichalwe amesema kati ya mabucha 235 yaliyokaguliwa 16 yamekutwa yanakiuka sheria zikiwemo za usafi na kuuza nyama zisizopimwa.

Aidha Bw.Sichalwe ameongeza kuwa pia lipo tatizo la baadhi ya mabucha yaliyofungiwa kuendelea kufanyakazi huku  wakichanganya aina mbalimbali za nyama suala ambalo ni kinyume cha sheria na baadhi yao wamekamatwa na kutozwa faini.

Kwa upande wao baadhi ya walaji wamewaomba wakaguzi kuweka utaratibu wa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwani baadhi ya watendaji wa serikali wasio waaminifu wanafumbia macho ukiukwaji wa sheria unaofanywa na baadhi ya wauza nyama.

Malalamiko ya wananchi ya kuwepo kwa baadhi ya wauza nyama yamekuwa yakitolewa mara kwa mara hasa suala la kuchanganyiwa aina tofauti  za nyama.