Back to top

"Rais ameteua vijana mnagombana aibu" -Majaliwa.

16 September 2019
Share

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amechukizwa na mgongano uliopo kati ya Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Majura Kasika na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo Mussa Mnyeti, hivyo kumuelekeza Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora kwenda kuchunguza weledi wa utendaji kazi  wao.

Waziri Mkuu ametoa maelekezo hayo leo (Jumatatu, Septemba 16, 2019) wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Malinyi pamoja na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Toboa, akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro.

Amesema Serikali imewapa nafasi hiyo ili wakasimamie maendeleo ya wananchi na inapeleka fedha kwa ajili ya kuboresha maendeleo ya jamii kama kuimarisha huduma za afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara lakini wao wanagombania miradi na mingine wanaichakachua.

Awali, Mbunge wa Jimbo la Malinyi, Dkt. Haji Mponda alimweleza Waziri Mkuu kwamba kwenye wilaya hiyo kuna matatizo ya mahusiano kati ya Serikali na Halmashauri jambo linalosababisha kukwama kwa shughuli za maendeleo.

Mbunge huyo alisema kutoelewana kwa viongozi wa wilaya hiyo Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi kumesababisha mgawanyo mkubwa kuanzia katika Baraza la Madiwani hadi kwa wananchi mitaani, hivvyo alimuomba Waziri Mkuu awasaidie katika. Kilipatia ufumbuzi suala hilo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu  amesema kuwepo kwa mabango mengi kwenye mikutano ya hadhara  ya viongozi wakuu kunadhihirisha wazi kwamba watendaji wa Halmashauri hawawatembelei  wananchi katika maeneo yao na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.