Back to top

Rais Dkt.Magufuli aondoka nchini kuelekea Afrika Kusini

24 May 2019
Share

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 24 Mei, 2019 ameondoka nchini kwenda Afrika ya Kusini ambapo kesho atahudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais Mteule wa nchi hiyo, Mhe. Cyril Ramaphosa.

Katika safari hiyo Mhe. Rais Magufuli ameongozana na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg. Philip Mangula na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi.

Wakizungumza kabla ya kuondoka, Mhe. Rais Mstaafu Kikwete na Makamu Mwenyekiti wa CCM Ndg. Mangula wamesema Tanzania na Afrika ya Kusini zina uhusiano mkubwa na wa kihistoria na kwamba Serikali na chama zina kila sababu ya kudumisha uhusiano na ushirikiano huo.

Viongozi hao wameondoka katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam kwa kutumia ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amesema baada ya kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais Mteule wa Afrika ya Kusini, Mhe. Rais Magufuli atafanya Ziara Rasmi ya Kitaifa nchini Namibia ambako pia atazindua mtaa uliopewa jina la Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere kwa kutambua mchango mkubwa alioutoa katika ukombozi wa Taifa hilo.