Back to top

Rais Magufuli aagana na Kagame, atoa neno siku ya wanawake.

08 March 2019
Share

Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame leo tarehe 08 Machi, 2019 amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku 2 hapa nchini Tanzania na kurejea nchini kwake, baada ya hapo jana kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Mhe. Rais Kagame ameagwa na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli.

Mara baada ya kuagana na mgeni wake, Mhe. Rais Magufuli amesalimiana na wananchi wa Dar es Salaam waliojitokeza kumuaga Mhe. Rais Kagame ambao wengi wao walikuwa ni wanawake na kuwatakia heri ya Siku ya Wanawake ambayo huadhimishwa tarehe 08 Machi, kila mwaka duniani kote.

Katika salamu hizo, Mhe. Rais Magufuli amewashukuru wanawake wote hapa nchini kwa mchango wao mkubwa kwa Taifa na amesema Serikali inatambua na kuthamini juhudi zao mbalimbali.