Back to top

RC Kagera awaombea wakulima mikopo kwa benki ya Posta Tanzania.

21 June 2019
Share

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti ameiomba Benki ya Posta Tanzania kuangalia uwezekano wa kutoa mikopo midogo kwa wakulima wa kahawa katika mkoa huo, ili iweze kuwaondolea vishawishi vya kuuza zao hilo kwa walanguzi kutoka nchi jirani wakati wakisubiri kuanza kwa msimu wa ununuzi wa kahawa.

Mkuu huyo wa mkoa ametoa ombi hilo, baada ya kuzindua tawi la benki hiyo katika wilaya ya Karagwe.

Amesema wakulima wa zao hilo wakati mwingine hulazimika kuuza kahawa yao kwa njia ya magendo ili waweze kutatua matatizo mbalimbali waliyonayo ambayo ni pamoja na kulipa ada za shule pamoja na pesa ya kujikimu kimaisha.

Wakati wa uzinduzi wa tawi hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo, Dakta Edmund Mndolwa amesema benki imeweka kipaumbele cha kuwasaidia wajasiliamari wadogo na kuahidi kuwa kulifanyia kazi ombi lililotolewa na mkuu huyo wa mkoa na baadhi ya wananchi waliozungumza wameomba benki hiyo ipanue wigo wake hadi maeneo ya vijijini.