Back to top

SERIKALI KUSHIRIKISHA VIJANA KUPAMBANA NA UHALIFU, BASHUNGWA ATOA ONYO

14 December 2024
Share

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mh. Innocent Bashungwa amesema Wizara kupitia vyombo vya usalama na taasisi nyingine za Serikali, zitashirikiana na Vijana ili kupata suluhu kwa baadhi ya changamoto zilizopo na zinazoendelea kujitokeza katika jamii, ikiwa ni pamoja uhalifu, kupambana rushwa, dawa za kulevya na Unyanyasaji wa kijinsia.


Waziri Bashungwa ameyasema hayo wakati akimwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko katika ufunguzi wa  Mkutano Mkuu wa Skauti Tanzania uliofanyika katika Ukumbi wa Pius Msekwa Bungeni, jijini Dodoma.


"Tuna nia ya dhati kushirikiana na Vijana wa Skauti katika kushughulikia masuala ya kihalifu, nina amini kabisa kupitia jukwaa hili tutaweza kwenda kwa jamii kupitia mafunzo na utimamu mlio nao kuifanya nchi izidi kuwa bora ya amani na usalama” amesema Bashungwa.


 Naye,  Rais wa Chama cha Skauti Tanzania ambaye pia ni Waziri wa Elimu,  Prof. Adolf Mkenda amesema kazi kubwa ya skauti ni kukuza na kulinda maadili ya Mtanzania, kuendeleza ujasiri hasa kwa vijana kujishughulisha na shughuli za maendeleo kwa jamii.


Kwa Upande wake, Skauti Mkuu wa Tanzania, Rashid Kassim Mchata amesema dhumuni la Mkutano huu ni kupitisha rasimu ya mabadiliko ya Katiba ya chama ili kukidhi mahitaji ya sasa na kupitisha sera mbalimbali za chama.