Back to top

Taasisi za fedha zinachangia kukwamisha biashara nchini.

07 June 2019
Share

Rais wa Tanzania Mhe.John Pombe Magufuli amesema idadi kubwa ya taasisi za udhibiti serikalini ni chanzo namba moja cha kukwamisha  biashara Tanzania.

Akifungua mkutano wa Baraza la Biashara la Taifa jijini Dar es salaam, ametaja changamoto nyingine kuwa ni wingi wa kodi, tozo, ushuru na ada zinazotozwa katika sekta mbalimbali hasa katika utalii, ngozi, nyama na mafuta ya kula.

Rais ameitaja changamoto ya tatu inayosababishwa na serikali kuwa ni rushwa hasa bandarini, Mamlaka ya Mapato na vizuizi barabarani na mipakani.

Aidha amesema taasisi za fedha zinachangia kukwamisha biashara kwa kuweka riba kubwa na masharti magumu kwa wakopaji.

Kwa upande wa wafanyabiashara Rais amesema baadhi yao siyo waaminifu kwani wanakwepa kodi na kutoa rushwa.

Amesema wengine wamebinafsishiwa viwanda na ardhi na hawakuendeleza na kuvitumia kukopa kwa mambo mengine.

Rais ametaja pia mauzo hewa, biashara hewa na manunuzi hewa kama kikwazo cha biashara ambapo ameonesha orodha ya kampuni 17,447 yanayotuhumiwa na mambo hayo na kuyapa siku 30 kujitathimini na watakaobainika kulipa mara moja.

Amewataka wafanyabiashara kuzungumza kwa uwazi, ili kupata jibu na mustakabali wa maendeleo ya nchi.