Back to top

TAKUKURU yamnasa Afisa wa Tanesco kwa tuhuma ya kuomba rushwa ya ngono

10 July 2019
Share

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Mtwara imemkamata Afisa Utumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani humo, Bwana Jumanne Songoro kwa tuhuma ya kuomba rushwa ya ngono ili ampangie mlalamikaji majukumu mengine mapya ya kazi kwenye shirika hilo.

Kamanda wa TAKUKURU Mkoani Mtwara, Bwana Stephen Mafipa amesema mtuhumiwa alianza kushawishi rushwa ya ngono kutoka kwa mlalamikaji tangu Desemba mwaka jana, ili ampangie majukumu mengine mapya ya kazi kulingana na elimu yake baada ya kubadilishwa majukumu ya awali na makao makuu ya shirika hilo.

Hata hivyo muda mfupi baadae mtuhumiwa Jumanne Songoro alifikishwa mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Bwana Hussein Mareng na kusomewa mashitaka na waendesha mashitaka wa TAKUKURU, Bwana Hassan Dunia na Nimrod Mafwele akishtakiwa kwa kosa la kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa kuomba rushwa ya ngono kinyume na cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya 2007.

Mshtakiwa alikana shtaka hilo na shauri hilo limeahirishwa hadi tarehe 23 mwezi itakapotajwa tena na mshtakiwa amerudishwa rumande kwa kukosa dhamana.