Back to top

Tanesco yawaonya wanaobandika Matangazo kwenye Miundombinu ya Umeme.

10 July 2019
Share

Shirika la ugavi wa umeme Tanzania (TANESCO), limetoa onyo kali kwa watu wanaobandika mabango na matangazo kwenye nguzo za umeme na miundombinu mingine ya Shirika hilo, kwani ni kinyume cha sheria na pia inahatarisha maisha yao kwani umeme ni hatari.

Akizungumza na Idara ya Habari (MAELEZO), katika mahojiano maalum Kaimu Meneja Uhusiano wa Shirika hilo Leila Muhaji, amesema Tanesco kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi watawachukulia hatua wale wote watakaobainika kukiuka maagizo hayo.


Kaimu Meneja uhusiano huyo wa TANESCO ameongeza kuwa wananchi wenye tabia hiyo ni bora wakaacha mara moja, kwani kwa kushirikiana Jeshi la Polisi wameshaanza kufanya msako kwenye maeneo mbalimbali sambamba na kubaini wanaoiba umeme wakishirikiana na vishoka.

Aidha alisema katazo hilo pia, linawahausu hata wale wenye mazoea ya kutundika bendera kwenye nguzo za umeme, pamoja na wote wanaohujumu miundombinu ya Tanesco kwa ujumla kuwa wakati wa kubembelezana sasa umekwisha, hivyo kila mtu mwenye mapenzi mema na nchi yake ahakikishe
anashiriki katika kulinda rasilimali za shirika hilo la umma.