Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa, amesema Wizara yake inaandaa mfumo kabambe wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambao utakuwa muarubaini wa changamoto zote za kimfumo katika sekta ya ardhi.
Waziri Silaa amesema hayo Jijini Arusha wakati alipokutana na timu ya wataalamu wa TEHAMA kutoka Wizara ya Ardhi na Taasisi mbalimbali wanaoandaa mfumo kabambe na unganishi wa kutunza na kuchakata taarifa za ardhi.
Amesema mfumo huu ndio majibu ya changamoto zote zinazoikabili sekta ya ardhi pamoja na sekta nyingine chini za Kilimo, Madini, Barabara, Umeme, Uwekezaji, Maji, Hifadhi, Mawasiliano na hata katika kufanya utafiti na upatikanaji wa takwimu.
Aidha, amesema kupitia mfumo huu suala la changamoto za migogoro ya ardhi itapatiwa ufumbuzi ikiwemo upatikanaji namba ya malipo (Control Number), malipo ya ada mbalimbali, upatikanaji hati, upimaji na Ramani, uthamini na hata upangaji wa makazi na nyumba.