Wakulima wa mazao ya mbogamboga katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa kaskazini wameingiwa na hofu ya kupata mavuno yasiyokidhi gharama wanazotumia kutokana na kuonekana kwa ugonjwa wa mnyauko unaoathiri zao la Nyanya.
Wakulima katika kijiji cha Kikwe kilichopo wilayani Arumeru ni miongoni mwa walioathiriwa na ugonjwa huo wakieleza kuwa wanalazimika kujaribu dawa za aina mbalimbali kukabiliana nao ambazo hata hivyo wataalamu wa kilimo wanawashauri kutokuzitumia bila kupata maelekezo ya kitaalamu.
Ugonjwa huo wa mnyauko unakuja wakati bado ugonjwa wa nyanya unaojulikana kama Kanitangaze ukiwa haujapatiwa suluhisho la kudumu,huku wakulima hao pia wakieleza kukabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa maji hususani wakati wa msimu wa kiangazi
Akizungumzia changamoto ya upatikanaji wa maji kwa ajili ya umwagiliaji wakati wa maonyesho ya siku ya mkulima iliyofanyika katika moja ya shamba darasa la kilimo cha nyanya lililopo kijijini kikwe,mkurugenzi mtendaji wa asasi kilele inayoendeleza kilimo cha horticulture hapa nchini –TAHA Jackiline Mkindi anasema jitihada zinafanyika kwa kushirikiana na wadau kuwajengea uwezo wakulima kutumia teknolojia ya umwagiliaji kwa njia ya matone