
Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan, ameiagiza Wizara ya Kilimo, kuisimamia kwa ukaribu Sekta ya Ushirika, ili uwekezaji unaofanywa na Serikali kwenye sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, uweze kufanywa na Vyama vya Ushirika.
Rais Dkt. Samia ametoa agizo hilo leo, katika kikao na Maafisa Ugani na wanaushirika kilichofanyika Ikulu, Chamwino.
Rais Dkt.Samia amesema serikali ina dhamira ya kurudisha hadhi ya ushirika Hususani, ushirika wa mazao hivyo ametaka ushirika uendeshwe kisasa, uwekezaji ufanywe kitaalam na ukiwa na lengo la kumnufaisha mwanaushirika moja kwa moja.
Vile vile, Rais Dkt. Samia amevitaka Vyama vya Ushirika kutokuwa sehemu ya kumyonya mwanaushirika, bali viwe mstari wa mbele kuwalinda na kuwatetea.
Rais Dkt. Samia amevielekeza vyama vya ushirika kuwa chachu ya mabadiliko na vyenye kuleta mageuzi ya fikra, ikiwemo kuchangia maendeleo mapana kwa kuhamasisha wanaushirika waweze kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii na Mfuko wa Bima ya Afya kwa wote.
Aidha Rais Dkt.Samia ameagiza Maafisa Ugani na Maafisa Ushirika kuhakikisha kuwa ruzuku ya
pembejeo inayotolewa na Serikali inaleta matokeo makubwa zaidi, kuwafikia wananchi vijijini
pamoja na kuwaelimisha mbinu bora za kilimo, ufugaji na uvuvi.
