Back to top

WAFUGAJI PWANI WAUNGA MKONO JUHUDI ZA RAIS SAMIA

27 August 2024
Share

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega. amewapongeza wafugaji wa Kijiji cha Mpelumbe, Kata ya Gwata, Walayani Kibaha, mkoani Pwani kwa kujitolea kujenga bwawa la kunyweshea mifugo yao.

Waziri Ulega ametoa pongezi hizo, wakati alipowatembelea wafugaji hao kuona juhudi wanazozifanya ambazo moja kwa moja zinaunga mkono jitihada za Mhe.Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuboresha sekta ya mifugo, ili iwe na mchango mkubwa kwa taifa na mtu mmoja mmoja.

"Nawapongezeni sana, na nitakwenda kumjulisha Mhe. Rais kuhusu jitihada zenu hizi, kwa kweli mmefanya kazi nzuri sana na sisi wizara tunakwenda kuwaweka katika mipango yetu kuanzia mwezi wa 12 hadi wa kwanza mwakani tutawapatia kiasi cha Milioni 50, ili ziwasaidie kuboresha bwawa hili mliloanza wenyewe kulitengeneza"Amesema Ulega.

Aidha, Waziri Ulega alitumia nafasi hiyo pia kuwaelimisha juu ya Kampeni ya TUTUNZANE iliyozinduliwa na Mhe. Rais Samia mkoani Morogoro inayohamasisha ufugaji wa kisasa ikiwemo kulima malisho, kuchimba mabwawa na kutunza mazingira.

Halikadhalika aliwahimiza wafugaji hao kuwa na maeneo yao kwa ajili ya kulima malisho aina ya Juncao kwa ajili ya mifugo yao huku akiwakabidhi mbegu aina ya rhodes ili wapande katika maeneo yao.