Back to top

Wapigadebe, mamalishe kituo kikuu cha mabasi mbeya kushonewa sare

07 May 2018
Share

Mkuu wa mkoa wa Mbeya ameiagiza halmashauri ya jiji la Mbeya kuwatambua vijana na mama lishe wote katika kituo kikuu cha mabasi jijini Mbeya na kisha kuwashonea sare na kuwawekea utaratibu mzuri wa kufanya shughuli zao ndani ya kituo hicho  kwa lengo la kuepusha uhalifu na kuwajengea mazingira mazuri ya kujipatia kipato kwa njia halali.

Mkuu wa mkoa wa mbeya, Amos Makalla ametoa agizo hilo  wakati akizindua jengo la abiria katika kituo kikuu cha mabasi jijini Mbeya ambalo limekarabatiwa na halmashauri ya jiji la Mbeya kwa kushirikiana na wadau, baada ya hapo awali jengo hilo kuonekana limechakaa na kuhatarisha maisha ya wananchi kwenye kituo hicho.

Awali diwani wa kata ya sisimba, Mhe. Geofrey Kajigili amesema usalama wa watumiaji wa kituo hicho cha mabasi sio mzuri hasa nyakati za usiku kutokana na taa kuharibika pamoja na choo cha stendi kuwa kibovu kisichoendana na hadhi ya kituo hicho cha mabasi.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji la Mbeya, Dkt. Amani Kilemile amesema tayari halmashauri yake imeshaziona changamoto za kituo hicho na imejiwekea mikakati ya kuzishughulikia kadri fedha zinavyopatikana.

Baada ya kusikiliza changamoto hizo, mkuu wa mkoa wa Mbeya, Amos Makalla ametoa siku 14 kwa halmashauri ya jiji la Mbeya kumweleza hatma ya changamoto hizo sambamba na mikakati ya kuziondoa, hatua ambayo imewafurahisha vijana kituoni hapo na kuamua kumsindikiza kwa kusukuma gari lake hadi nje ya stendi hiyo.