Back to top

Watu 73 washikiliwa na polisi mkoani Shinyanga kwa Uhalifu

18 August 2019
Share

Jeshi la polisi mkoani Shinyanga limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne wa matukio ya mauaji ya watu wawili wa familia moja na wengine zaidi ya 70 waliokamatwa wakijihusisha na uhalifu mbalimbali ikiwemo kusafirisha dawa za kulevya,utekaji,wizi na utengenezaji wa pombe haramu ya moshi.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Shinyanga ACP Richard Abwao amewataja watuhumiwa wanne kati ya 73 wanaoshikiliwa kwa tukio la kufanya mauaji ya mwanamke mmoja kwa kumfungia mawe shingoni na miguuni na kumtumbukiza kwenye lambo la maji kwa lengo la kupoteza ushahidi huku wakiwa wamemteka mtoto wake na kusafiri naye hadi wilayani Mpanda mkoani Katavi kumuua na kutelekeza mwili wake porini ambapo uliliwa na fisi na kubakizwa mabaki tukio ambalo linadaiwa chanzo chake ni kuwania mali.

Aidha kamanda Richard Abwao amesema katika kipindi cha mwezi mmoja jeshi la polisi mkoani Shinyanga limefanikiwa kukamata watuhumiwa waliokuwa wamepora pikipiki na kuwaua madereva wake huku wakikamata vifaa vya kuvunjia milango na mageti ikiwemo silaha hatari ya kienyeji ya kukaba shingo za watu wakati wakitekeleza uhalifu.

Hata hivyo kamanda Richard Abwao ameseam watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani punde upelelezi utakapomalizika huku akitoa wito kwa wakazi wa mkoa wa Shinyanga kutoa taarifa mapema endapo wakiona dalili zozote za uhalifu na kuwataka watu wanaojihusisha na uhalifu kuacha mara moja.