Back to top

Watumishi 6 wa idara ya afya Ukerewe washikiliwa kwa tuhuma za wizi

12 October 2019
Share

Watumishi sita wa idara ya afya wilaya ya ukerewe mkoani Mwanza, akiwemo mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya hiyo Dkt.Titus Kaniki pamoja na mganga mkuu wa wilaya hiyo Dkt.Raphael Mhana wanashikiliwa  kwa tuhuma za wizi wa dawa zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 400, ambazo wamekuwa wakiziagiza kutoka bohari ya dawa (MSD) kanda ya ziwa kwa kutumia mfumo usio rasmi.

Tuhuma hizo zimebainishwa na mkuu wa wilaya ya Ukerewe Cornel Magembe, wakati akizungumza na watendaji na viongozi wa serikali wilayani humo katika kikao kazi cha kujadili changamoto za ukusanyaji wa mapato katika halmashauri ya wilaya hiyo.

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa wilaya ametoa siku 14 kwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Ukerewe Esther Chagula, mweka hazina pamoja na mkusanya mapato kurudisha zaidi ya shilingi milioni 481 za halmashauri hiyo za kuanzia mwaka 2015/2016 hadi mwaka 2019/2020 ambazo hazijulikani zilipo

Mbunge wa jimbo la Ukerewe Joseph Mkundi amesikitishwa na upotevu wa fedha hizo kutokana na ukosefu wa maadili kwa baadhi ya watumishi wa halmashauri ya wilaya hiyo, huku mwenyekiti wa halmashauri hiyo George Nyamaha akiwataka watendaji kuwasimamia ipasavyo wakusanyaji wa mapato ya serikali.