Back to top

Waziri mkuu amtaka mtendaji mkuu tba ajitathmini

18 November 2019
Share

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemtaka Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Arch. Daud Kondoro ajitathmini kuhusu utendaji kazi wake huku akiwasimamisha kazi wakurugenzi watatu wa wakala huo.
 
“TBA tunaihitaji lakini watu wake wana shida. Hatuwezi kuwaacha, TBA wasipewe miradi kwa sababu hawawajibiki na wanadhani kwa kuwa ni taasisi ya Serikali ndio wataachwa wafanye mambo ya hovyo.”
 
Waziri Mkuu amewasimamisha kazi wakurugenzi hao leo wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) eneo la Njedengwa jijini Dodoma.
 
Wakurugenzi waliosimamishwa kazi ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ujenzi, Arch.Humphrey Killo, Kaimu Meneja wa Miradi, Abdallah Awadh na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ushauri Arch. Hamis Kileo.
 
Waziri Mkuu amechukua hatua hiyo baada ya kutoridhishwa na utendaji kazi wa TBA katika miradi mbalimbali waliyopewa na Serikali ukiwemo ujenzi wa jengo la NEC ambalo ujenzi wake ulianza Julai, 2017 na ulitakiwa ukamilike Juni 2018 kwa gharama ya sh. bilioni 13. Hata hivyo mradi huo bado haujakamilika na ujenzi wake umesimama.