Back to top

MALECELA APONGEZA UIMARA WA CCM NA SERIKALI YAKE KUTUMIKIA WATANZANIA

05 December 2024
Share

Makamu wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu, Mzee John Malecela, amewataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuendelea kuwa na moyo wa kizalendo na kujituma kwa ajili ya maslahi ya taifa. 

Ameeleza haya baada ya kutembelewa nyumbani kwake Upanga Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, ambapo Malecela amepongeza chama hicho kwa kuendelea kuonesha uongozi imara chini ya Mwenyekiti wake, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Malecela ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Mstaafu (Bara), amesema utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa CCM, unaendelea kwa kasi na umedhihirisha dhamira ya kweli ya chama hicho kuwatumikia Watanzania. 

Amebainisha kuwa mafanikio ya Rais Dkt. Samia, hususan katika sekta za maendeleo ya miundombinu, afya, na elimu, yanapaswa kuwa chachu ya wanachama kuendeleza mshikamano na kuimarisha uongozi wa chama, ambacho kimejengwa juu ya misingi imara ya kutumikia watu. 

"Wanachama wa CCM wanapaswa kuwa mfano bora wa uzalendo kwa wengine. Hili ni jukumu letu la kihistoria, ambalo tunapaswa kuliheshimu kwa vitendo"Amesema Malecela.

Kwa upande wake, Balozi Nchimbi amemshukuru Malecela kwa mchango wake wa mawazo na uzoefu unaoendelea kuwa hazina kubwa kwa Chama na Serikali.

Amesema viongozi wastaafu kama Malecela wamekuwa mstari wa mbele kutoa ushauri unaosaidia kuimarisha utendaji wa chama katika nyanja mbalimbali.

"Uzoefu wenu ni mwanga kwetu. Tunaendelea kuthamini mawazo yenu ambayo yamekuwa nguzo muhimu kwa chama na taifa kwa ujumla"Amesema Nchimbi.

Katika mazungumzo hayo, Malecela pia ametoa wito kwa wanachama wa CCM kuendeleza mshikamano na maadili ya chama, akisisitiza kuwa hiyo ni mojawapo ya misingi ya mafanikio ya CCM kwa zaidi ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwake.

Amewaasa viongozi wa sasa wa CCM kuendeleza kazi nzuri wanayoifanya huku wakizingatia misingi ya haki, uwazi, na uwajibikaji. 

Amesema maadili ya uongozi bora yamekuwa kichocheo kikubwa cha imani ya wananchi kwa CCM.

"Huu ni wakati wa kuchapa kazi zaidi, kuhakikisha tunazidi kuimarisha maendeleo ya nchi yetu huku tukiheshimu dhamira kuu ya chama ya kuwatumikia wananchi"