Back to top

KITUO CHA AFYA KIBAONI HALMASHAURI YA MPIMBWE CHAPATA GARI LA WAGONJWA

06 May 2024
Share

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa jimbo la Kavuu katika Halmashauri ya Mpimbwe Wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi Mhe.Geophrey Pinda, amekabidhi gari la wagonjwa kwa ajili ya Kituo cha Afya Kibaoni.

ZOezi hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Mlele akiwemo Mkuu wa Wilaya hiyo Alhaji Majid Mwanga na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mpimbwe Bi.Shamim Daud, ambapo kukabidhiwa kwa gari hilo kunaifanya Halmashauri ya Mpimbwe kuwa na jumla ya magari matatu ya kubebea wagonjwa yanayohudumia vituo vya afya vya Kibaoni na Usevya huku gari moja ikihudumia hospitali ya Wilaya ya Tupindo.

Naibu Waziri wa Ardhi Mhe.Pinda amewaomba wananchi wa kibaoni kuitumia gari hiyo huku akimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mpimbwe kuhakikisha gari waliyokabidhiwa inabakia kwa matumizi ya kituo hicho cha afya cha Kibaoni.

Gari hilo linaenda kuongeza uwezo kwa kituo hicho cha afya kwa kuwa mtu akipata rufaa kutoka Kibaoni kwenda Hospitali ya wilaya mafuta hayatatumika sana tofauti na hapo awali ambapo ililazimika mgonjwa kupelekwa sumbawanga.

Upatikanaji gari la wagonjwa kwenye Kituo cha Afya Kibaoni kutasaidia kutatua changamoto za usafiri sambamba na kurahisisha huduma za dharura kwa maeneo jirani na hiyo inatokana na kuongezeka kwa mahitaji  katika eneo la Kibaoni kama vile uwepo wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda.

Wananchi wa Kibaoni wamemshukuru Mbunge wa jimbo la Kavuu Mhe.Geophrey Pinda kwa kusaidia upatikanaji wa gari hilo la wagonjwa pamoja na fedha za ujenzi wa kituo cha afya cha Kibaoni.

Kwa mujibu wa taarifa ya Halmashauri ya Mpimbwe, mwezi Januari 2024 kituo hicho kilipokea shilingi milioni 175 kutoka serikali kuu kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba pamoja na umaliziaji majengo ya Maabara, Jengo la Mama na Mtoto, Upasuaji na Kichomea Taka.

Ukamilishaji wa kituo cha Afya Kibaoni utatoa huduma kwa wananchi takriban 28,817 wa kata ya kibaoni na viunga vyake.