Back to top

KUANZIA SASA SABAYA HANA REKODI YA UHALIFU

03 May 2024
Share

Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini(DPP) Silvester Mwakitalu, leo amewasilisha katika Mahakama Kuu ya Tanzania masijala ya Arusha, ombi la kuiondoa rufaa no.155 ya mwaka 2022 aliyokua ameikata dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake.
.
Rufaa hiyo ilikatwa na Jamhuri baada ya Sabaya na wenzake kushinda kesi hiyo ya uhujumu uchumi no.27 ya mwaka 2021 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, iliyosikilizwa na kuamuliwa na Hakimu Patricia Kisinda.
.
Rufaa hiyo ilipangwa kusikilizwa mfululizo na mahakama kuu kuanzia Aprili 29, 2024 hadi Mei 03, 2024, mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam, Mhe.Salma Maghimbi aliyefika kusikiliza shauri hilo.
.
Akiwasilisha nia ya kuliondoa shauri hilo mbele ya Mhe. Jaji Salma Maghimbi, Muendesha Mashtaka Muandamizi wa Serikali, Akisa Mhando alieleza kuwa “Mhe Jaji, shauri hili limekuja kwa ajili ya kusikiliza rufaa, hata hivyo mrufani (Jamhuri) imewasilisha ombi chini ya kifungu cha sheria no.386 (1) cha sheria ya muenendo wa makosa ya jinai marejeo ya mwaka 2022, ombi letu ni kwamba Jamhuri haina nia ya kuendelea na rufaa hii dhidi ya Sabaya na wenzake, hivyo tunaomba kuiondoa hapa mahakamani”.


Baada ya uamuzi huo, Jaji Maghimbi alitoa uamuzi kwamba rufaa hiyo imeondolewa Mahakamani rasmi.
.
Kufuatia uamuzi huo, Sabaya anakuwa hana shauri lolote linalomkabili mahakamani na anahitimisha rasmi leo safari ya kesi alizokuwa anakabiliana nazo tangu Juni 04, 2021 alipopandishwa kizimbani mara ya kwanza.
.
Wakili wa Sabaya, Moses Mahuna, amewaambia Waandishi wa habari kuwa kuanzia sasa, Sabaya ni mtu huru na kwa mujibu wa mahakama yenyewe, hana rekodi yotote ya uhalifu na hana shauri lingine lolote katika chombo chochote cha sheria, na kumfanya kumalizana rasmi na mahakama.