Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuhakikisha linatekeleza kwa kasi miradi ya umeme itakayounganisha Mkoa wa Kigoma, katika gridi ya Taifa ifikapo mwishoni mwaka huu ili Mkoa huo usitumie umeme unaozalishwa kwa kutumia mafuta mazito.
Ametoa agizo hilo mkoani Kigoma, wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi mradi wa uzalishaji umeme katika mto Malagarasi (49.5 MW), uwekaji wa jiwe la msingi mradi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kV132 kutoka Igamba hadi Kidahwe na Kituo cha kusambaza umeme msongo wa kV 400/220/132/33 cha Kidahwe.
Amesema kuwa, Serikali imekuwa ikitumia shilingi bilioni 35 kwa mwaka kwa ajili ya kununua mafuta kwa kuendeseha majenereta ya kuzalisha umeme huku makusanyo yakiwa ni shilingi bilioni 16 hivyo imekuwa ni hasara kwa Shirika.
Amesema zoezi hilo la uzimaji wa majenereta pia litafanyika kwa mikoa ambayo haijafikiwa na umeme wa gridi.
Ameeleza kuwa, Kigoma inaingia kwenye historia ya kuwa na umeme wa uhakika wa gridi kwa kuwa itapata umeme kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo kutoka Nyakanazi kwa msongo wa kV 400 na kV 220, njia nyingine ni kutoka chanzo cha Malagarasi hadi Kidahwe, kutokea Katavi kwa msongo wa kV 400 na laini ya SGR kutoka Dar es Salaam ya kV 220.
Dkt. Biteko amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Kigoma ambapo katika Sekta ya Nishati ametoa zaidi ya shilingi trilioni 1.2 katika mwaka wa fedha 2024/2025 ili kutekeleza miradi ya umeme.
Ameeleza kuwa, kwa umeme wa gridi kufika Kigoma Mkoa huo sasa unaondoka kwenye historia ya kuitwa mkoa wa pembezoni na kutambulika kama Mkoa wa maendeleo.
Kuhusu kazi ya usambazaji umeme vijijini amesema Vijiji vyote vitapata umeme kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Katika hatua nyingine Dkt.Biteko ametoa mifuko 500 ya simenti ili kuunga mkono juhudi za wananchi ambao wameanza kujenga kituo cha afya katika Kata ya Kidahwe huku akiahidi kuwa Serikali itajenga kituo kingine cha afya.
Aidha katika Kijiji cha Igamba ambapo kunatekelezwa mradi wa Malagarasi amesema itajengwa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo Barabara ya lami ya kilometa 20 .
Dkt. Biteko pia ameipongeza TANESCO kwa kubadilika katika utrendaji kazi kwa kujikita katika kupelekea watu umeme ambapo amewataka wasirudi nyuma na kwamba anaona fahari kuongoza Shrika hilo kwa sasa.
Aidha, kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa amewaasa wananchi kuchagua viongozi kutokana na uwezo wao wa kuwahudumia na siyo kigezo cha fedha.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mhe. Zainabu Katimba amesema Mkoa wa Kigoma umepokea shilingi trilioni 11.5 kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika kipindi cha uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwemo sekta ya Nishati ambayo imepata zaidi ya shilingi Trilioni moja.
Amesema uwekezaji wa miradi hiyo ya umeme una tija kwani umeme unahitajika katika maeneo mbalimbali mkoani humo ikiwemo Shule 983, Vituo vya Afya 324 na Hospitali za Halmashauri hasa wodi za watoto wachanga na Watoto njiti ambapo kuna vifaa vya kisasa vyenye mahitaji ya umeme.
Ameeleza kuwa, uwekezaji huo unaonyesha kuwa umeme mkoani Kigoma unafika kwa kishindo na kumpongeza Dkt. Biteko na uongozi Wizara ya Nishati kwa kufanya kazi kubwa na za kimkakati na kitalam zinazoendelea kuboresha Sekta ya Nishati.
Ameendelea kuwaasa wananchi kufuatilia ratba zote za ucjaguzo wa serikali za mitaa tarehe 11 hadi 20mwezi huu kutakapokuwa na zoezi la kujiandikisha katika daftari la mkazi na kuchagua viongozi bora wanaoendana na kasi ya Rais Samia.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, CGF (Mst.) Thobias Andengenye amemshukuru Rais, Dkt. Samia kwa miradi ya maendeleo mkoani Kigoma ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake ya kuufungua Mkoa wa Kigoma na hivyo kuwa kitovu cha uchumi ambapo katika kipindi cha miaka mitatu na nusu cha uongozi wake ametoa shilingi trilioni 11 na bilioni 500 kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya umeme.
Ameahidi kuwa, Mkoa utasimamia vizuri fedha zinazotolewa ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amesema leo ni siku ya kipekee kwani kuzinduliwa kwa miradi hiyo kunaifanya Kigoma kuwa na uhakika wa umeme kwa kuwa kwa miaka mingi ulikuwa ni mmoja wa mikoa ya pembezoni huku sifa mojawapo ya mikoa hiyo ikiwa ni kutokuwa na umeme wa uhakika lakini kwa sasa ni sehemu kadhaa tu za mkoa huo hazipo kwenye gridi huku miradi ikiendelea.
Amesema Mkoa wa Kigoma sasa utaungwa kwenye gridi kwa kutumia njia saba tofauti za umeme ikiwemo laini ya kV 400 kutoka Nyakanazi, laini ya kV 400 kutoka Katavi, laini ya SGR ya kV220, laini ya kV 132 kutoka Malagarasi na mitambo ya umeme jua iliyopo mkoani Kigoma ambayo itapelekea Kigoma kuwa kitovu cha umeme nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga amesema lengo kuu la Mradi wa Umeme wa Malagarasi ni kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme wa uhakika Magharibi mwa Tanzania ikiwemo Kigoma ili kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi katika mikoa ya Magharibi mwa nchi ikiwemo Kigoma. Mradi huu utawezesha ongezeko la umeme katika Gridi ya taifa hivyo kuwezesha biashara ya umeme wa kikanda (Southern and Eastern Africa power pools),.pia zaidi ya wafanyakazi 700 wataajiriwa.
Amesema mradi wa Malagarasi utaimarisha hali ya usambazaji wa umeme katika mkoa wa Kigoma na Wilaya zake hivyo kupunguza gharama za uzalishaji wa umeme ambapo kwa sasa baadhi ya Wilaya za Mkoa wa Kigoma zinapata huduma ya umeme unaozalishwa kwa gharama kubwa kwa kutumia jenereta za mafuta ya Dizeli kutoka mitambo ya TANESCO iliyopo Kigoma mjini hali inayopelekea kuliongezea Shirika gharama za uendeshaji.
Ametaja gharama za jumla katika mradi wa Malagarasi ni Dola za Marekani milioni 144.14 (Sh.Bilioni 398) ambapo Serikali ya Tanzania inagharamia Dola za Marekani milioni 4.14 na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) inagharamia Dola za Marekani milioni 140 huku mkandarasi wa Bwawa na kituo cha kuzalisha umeme akiwa ni Dongfang Electric International Corporation kutoka China na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya kV 132 Igamba-Kidahwe (km 54) mkandarasi ni Shyama Power India Limited kutoka nchini India. Mradi pia utasambaza umeme kwenye vijiji 7 na kaya 750 zitaunganishiwa umeme.
Ameeleza kuwa, ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Kidahwe una sehemu mbili ambazo ni msongo wa kV 400 na msongo wa kV 220/132/33 ambayo itawezesha Mkoa wa Kigoma kuungwa kwenye gridi ya Taifa kutokea kituo cha Nyakanazi ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 87 huku mkandarasi akiwa ni kampuni ya Sean & Hyusong Consortium kutoka Korea.
Amemshukuru Rais, Dkt. Samia kwa kuipa kipaumbele sekta ya nishati huku mfano hai ni mradi wa umeme wa Julius Nyerere ( JNHPP) ambao unaingiza umeme kwenye gridi.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe.Kirumbe Ng'enda amemshukuru Rais Samia kwa fedha za utekelezaji wa miradi na kueleza kuwa, Taifa linakua kwa kasi kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo ya umeme kama JNHPP, Malagarasi, uendelezaji Gesi Asilia na usambazaji umeme.
Mohamed Sauko, Mwakilishi kutoka AfDB amemshukuru Rais kwa kushirikiana na Benki hiyo katka miradi mbalimbali ikiwe mo ya Reli, umeme na Barabara.
Ameishauri Serikali baada ya kuwa na umeme wa uhakika ijenge laini itakayoenda Burundi kwa ajili ya biashara ya umeme.