Back to top

68 WAHITIMU MAFUNZO YA UFUGAJI JONGOO BAHARI LINDI

31 March 2023
Share

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.David Silinde, amefunga mafunzo ya ufugaji Jongoo Bahari, yaliyokuwa yakifanyika kwenye chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kampasi ya Lindi na kuratibiwa na Wizara hiyo chini ya Wakala ya Mafunzo ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kampasi ya Mkindani mkoani Mtwara.

Mafunzo hayo yalihusisha washiriki 68 yamefanyika kwa muda wa siku 10 ambapo kwenye hotuba yake ya kufunga mafunzo hayo Mhe.Silinde amewataka kutumia ujuzi walioupata kuzalisha Jongoo Bahari wa kutosha ili kuongeza kipato chao na Taifa kwa ujumla.

"Mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa Maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa kwenye kilele cha Maonesho ya Nanenane mwaka jana mkoani Mbeya ambapo alielekeza sekta zote za uzalishaji ikiwemo sekta ya Uvuvi kushirikisha wadau mbalimbali ikiwemo sekta binafsi kuwawezesha wananchi waweze kujiajiri"Amesema Mhe.Silinde.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe.Shaibu Ndemanga mbali na kuishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kutekeleza ahadi yake ya kuwezesha mafunzo hayo , amewataka wananchi wote mkoani humo kujiingiza kwa wingi kwenye uzalishaji wa mazao ya Uvuvi ikiwemo jongoo bahari ili kuendelea kuupandisha uchumi wa mkoa kwa ujumla.

"Kilo moja ya Jongoo bahari inauzwa zaidi ya shilingi 180,000 sasa kama wananchi wote tutajikita kwenye shughuli hii bila shaka tutafia mbali sana na ninawaomba wenyeviti wa Halmashauri, Mstahiki Meya na wakurugenzi mliopo hapa, ile asilimia 10 ya wanawake na vijana ni bora wapewe wahitimu hawa wa mafunzo kwa sababu wanafanya shughuli ambayo inajulikana na faida yake inaonekana wazi"Amesema Mhe.Ndemanga.

Akielezea sababu ya kutoa mafunzo hayo ya Jongoo bahari, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Mafunzo ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Dkt. Semvua Mzighani amebainisha kuwa Taasisi yake iliamua kujikita kwenye mafunzo ya jongoo bahari kutokana na zao hilo la Uvuvi kuwa na thamani kubwa sana kwa hivi sasa.

"Na ukitaka kuthibitisha hilo angalia jinsi jongoo bahari walivyopungua kwenye vyanzo vya asili ndio maana tunawekeza kwenye ufugaji ili waweze kuongezeka na wananchi waweze kuongeza kipato chao na bahati nzuri wanafunzi wetu wamefundishwa jinsi ya kufuga, kuwakuza na kuwasindika mpaka watakapofika sokoni"Amesisitiza Dkt. Mzighani.

Naye mwakilishi wa wahitimu wa mafunzo hayo bi. Bishara Mabruk ameeleza kuwa mafunzo hayo yametolewa kwa weledi na ustadi kwa kila mada walizokuwa wakifundishwa ambapo amechukua fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha kuyapata bila malipo yoyote.