Back to top

"AFRIKA UPATIKANAJI WA NISHATI BADO NI MDOGO"

05 March 2025
Share

Makamu wa Rais, Mhe.Dkt. Philip Isdor Mpango amesema kuwa matumizi ya nishati katika Bara la  Afrika hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara  bado ni madogo ikilinganishwa na maeneo mengine kama Bara la Amerika, Asia na Ulaya hivyo kuna umuhimu wa kubuni njia bora za kuzitumia rasilimali zilizopo ikiwemo Mafuta na Gesi Asilia ili kuwawezesha wananchi kustawi kiuchumi na kijamii huku suala la utunzaji wa mazingira likizingatiwa.

Amesema hayo wakati akifungua rasmi Kongamano na Maonesho ya Petroli ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAPCE’25) ambalo litafanyika kwa muda wa Siku Tatu jijini Dar es Salaam.

“Katika kipindi ambacho maendeleo ya nishati endelevu yana mchango mkubwa katika mustakabali wa mazingira, uchumi na jamii zetu na katika kipindi ambacho Dunia inakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi bado tunahitaji  kutumia rasilimali zetu zilizopo, ikiwemo mafuta na gesi asilia lakini bila kuhatarisha mustakabali wa vizazi vijavyo ili kukidhi mahitaji ya kinishati.” Amesema Dkt. Mpango

Ameeleza kuwa, Afrika Mashariki imebarikiwa na rasilimali nyingi za nishati, ikiwemo mafuta na gesi asilia  ambapo  Tanzania imegundua gesi asilia, Uganda, Kenya na Sudan Kusini wamegundua mafuta, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wana gesi ya methane, huku Kenya na Tanzania zikiwa na rasilimali za nishati jotoardhi hivyo rasilimali hizo lazima  zitumike ili kupunguza pengo la nishati na kuharakisha maendeleo.

“Tunatambua kuwa ulimwengu unakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha madhara makubwa kama vile vipindi visivyotabirika vya mvua, mafuriko, mitetemeko ya ardhi na kuongezeka kwa joto. Tanzania, kama mataifa mengine, imejitolea kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa  ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kufanikisha azma ya kutozalisha hewa ya kaboni ifikapo mwaka 2050. Hata hivyo, tunapaswa kuweka uwiano kati ya ukuaji wa uchumi na uendelevu wa vyanzo vyetu  kwa kutatua changamoto za leo huku tukijiandaa kwa changamoto za kesho.” Amesema Dkt. Mpango

Dkt. Mpango ameeleza kuwa, suala la kuhama kutoka kwenye nishati chafu kwenda kwenye nishati safi haliepukiki  kwani ni mkakati muhimu wa kupunguza uchafuzi wa mazingira duniani hata hivyo uwekezaji katika nishati hiyo unahitaji mtaji mkubwa na utaalamu wa hali ya juu ambapo inakadiriwa kuwa Afrika inahitaji kati ya Dola Trilioni 1 hadi 2 kufanikisha malengo ya  ya kuelekea kwenye nishati safi ifikapo mwaka 2030 hivyo kuna umuhimu wa kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji na kuwa na ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekta ya umma.

Katika Mkutano huo wa EAPCE’25, Dkt, Mpango amesema kuwa anaamini Viongozi na Watalaam watabadilishana mawazo na uzoefu kuhusu kufungua fursa za uwekezaji katika nishati endelevu bila kusahau  nafasi ya rasilimali za mafuta katika upatikanaji wa nishati ya kutosha huku akisisitiza  ushirikiano wa kikanda kuelekea kwenye matumizi ya nishati safi.