
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeridhia Mpango wa Ununuzi wa Pamoja wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Pooled Procurement Services, SPPS) kwa kuwa ni nyenzo muhimu katika azma ya kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya na hivyo kuboresha afya na maisha ya wananchi wote wa nchi wanachama.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo katika Mkutano wa dharura wa Mawaziri wa Afya na Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya VVU na UKIMWI katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Uliofanyika kwa njia ya mtandao akiwa katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya Jijini Dar es Salaam.
"Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaamini kuwa, mpango huu wa pamoja ni nyenzo muhimu ya kutuunganisha katika azma ya jumuiya yetu katika kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya na hivyo kuboresha afya na maisha ya wananchi wetu, umoja wetu ni nguzo muhimu katika kulifikia hilo," amesema Waziri Mhagama
Aidha, Waziri Mhagama amesema, katika kuboresha mpango wa biashara uliowasilishwa, JMT inapendekeza maboresho madogo ili kuruhusu mifumo mitatu ya ununuzi wa pamoja (hybrid model) kutumika kwa pamoja katika miaka mitano ya kwanza badala ya kuanza na mfumo mmoja tu wa ununuzi wa makundi (group contracting).
"Hatua hii itasaidia kuongeza wigo mpana kwa nchi wanachama kuchagua mfumo inakayoona unafaa kwa mazingira ya nchi yake kwa wakati huo," amesema Waziri Mhagama
"Kama tunavyokumbuka, kupitia uamuzi wa Mawaziri wa Novemba 2017, Polokwane, Afrika Kusini, JMT iliteuliwa kuwa mwenyeji wa kudumu (host) wa mpango wa ununuzi wa pamoja, hivyo basi, JMT ipo tayari kushirikiana na nchi wanachama pamoja Sekretarieti ya SADC katika utekelezaji wa mpango huo wa ununuzi wa pamoja," amesisitiza Waziri Mhagama
Katika hatua nyingine, Waziri Mhagama amesema, Serikali ya JMT imekuwa ikitekeleza afua za kutokomeza Malaria kwa upande wa Zanzibar na Mikoa mitano ya Tanzania Bara ikiwemo Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Iringa na Njombe ambayo imefikia kiwango cha chini cha maambukizi ya Malaria cha chini ya asilimia 1.
"Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea na utekelezaji wa afua za kutokomeza Malaria kwa awamu ili kuweza kutokomeza ugonjwa huo wa Malaria nchini ifikapo mwaka 2030," amesema Waziri Mhagama
Mkutano huo ulikua na ajenda nyingine ikiwemo ya kujadilia namna ya kujikinga na magonjwa ya milipuko kama Marburg na Mpox, namna ya kutokomeza kifua kikuu pamoja na kuongeza kasi ya utekelezaji wa mkakati wa afya ya uzazi ambapo kwa Tanzania imeridhia kwa maazimio yote yaliyowasilishwa pamoja na maboresho yake.