Back to top

AVELINA JELA MIAKA 2 KOSA LA USAFIRISHAJI BINADAMU

23 July 2024
Share

Avelina Masini (19) Mkazi wa Kijiji cha Buzegwe kilichopo Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, amehukumiwa kulipa faini ya shilingi millioni tano au kutumikia kifungo cha miaka miwili gerezani baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la usafirishaji haramu wa binadamu.

Hukumu hiyo imesomwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Ukerewe, Mheshimiwa A.M.Bushiri ambapo amesema baada ya Mahakama hiyo kujiridhisha na ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri, shitaka limethibitishwa bila kuacha mashaka na kumkuta mshitakiwa na kosa.

Mwendesha Mashtaka wa Serikali Aidan Nziku, ameeleza mahakamani hapo kuwa Julai 15,2024 kwa nyakati tofauti tofauti mshitakiwa alitenda kosa hilo katika Kijiji cha Buzegwe kwa kuwatafuta watoto wa kike wawili wenye umri wa miaka 15 na 16, wanafunzi wa shule ya Sekondari na Msingi kwa lengo la kuwapeleka Jijini Mwanza na Mikoa mengine kufanya kazi za ndani (House girl).

Julai 15,2024 Mshitakiwa akiwa na waathiriwa kwenye Meli ya Mv.Nyehunge katika bandari ya Nansio/Ukerewe akiwa anataka kuelekea Jijini Mwanza, alikamatwa na askari wa Jeshi la Polisi na kufikishwa katika Kituo cha Polisi Nansio.

Aidha, Mwendesha mashtaka Nziku amesema mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 4(1)(a)(5)cha Sheria ya Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu Sheria Na.6 ya mwaka 2008.