
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Batilda Buriani, amewaambia wakazi wa Tanga kuwa ndani ya Miezi mitano tangu kutanuliwa na kuboreshwa kwa Bandari ya Tanga kulikofanywa na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, Jumla ya takribani Shilingi bilioni 100 zimepatikana kama faida inayotokana na bandari hiyo na hivyo kusisimua na kukuza uchumi wa mkoa huo na kanda nzima ya Kaskazini mwa Tanzania.
Mkuu wa Mkoa huo Mhe.Batilda ameeleza hayo mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, wakati wa Mkutano wa hadhara unaofanyika kwenye viwanja vya Mkwakwani Jijini Tanga, akimshukuru Rais Samia kwa kuikumbuka Tanga na kupeleka miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo ya takribani Trilioni 3.1
Wakati wa siku yake ya sita ya ziara Mkoani humo, Mhe. Batilda amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan pia kwa kurejesha ajenda ya viwanda Mkoani Tanga, akisema Ujenzi wa viwanda kilikuwa ni kilio cha muda mrefu kwa wakazi wa Tanga kwani kutasaidia pia kuongeza na kuzalisha fursa mpya za ajira kwa Vijana wa Tanga.
Utendaji wa Bandari ya Tanga, umeimarika kwa kiasi kikubwa katika miaka ya hivi karibuni kutokana na uwekezaji mkubwa wa serikali ambapo Bandari hiyo ilijengwa kwa mara ya kwanza mwaka 1914, ili kukidhi mahitaji ya kibiashara na kilimo kaskazini mwa Tanzania.
Ni bandari iliyopata uwekezaji mkubwa wa umma katika kipindi cha miaka minne iliyopita na kuiweka katika ramani ya kimataifa, kama kituo muhimu kwa meli kubwa.
Maboresho katika Bandari ya Tanga yalifanyika kwa awamu mbili ikiwa ni pamoja na kuongeza kina cha maji kutoka mita tatu hadi mita 13 na kupanua njia ya meli kugeuza. Mradi pia ulijumuisha ununuzi wa vifaa vipya vya kushughulikia mizigo na upanuzi wa gati mbili katika bandari hadi upana wa mita 450.
Maboresho hayo pia yameimarisha utendaji kazi wa Bandari ya Tanga, yakiwezesha bandari kupakua mizigo kutoka kwa meli kubwa ndani ya siku mbili, tofauti na siku tano au zaidi zilizokuwa zinahitajika awali.