Back to top

BARABARA ZILIZOATHIRIWA NA MVUA KUFUNGULIWA KWA WAKATI.

30 April 2024
Share

Serikali imesema itahakikisha  barabara zote zilizoathiriwa na mvua za El-Nino, ambazo zimeendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali  nchini, na kuleta uharibifu wa miundombinu ya barabara zinarejeshwa kwa wakati.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa  wakati alipotembelea na kukagua barabara ya Kibada-Mwasonga-Kimbiji katika Manispaa ya Kigamboni, akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili , jijini Dar es Salaam.

 Waziri Bashungwa amewahakikishia wananchi kote nchini kuwa hakuna barabara ambayo mawasiliano yatakatika kutokana na mvua kisha ikaachwa bila ya mawasiliano yake kurudishwa kwa haraka.

Kuhusu ujenzi wa barabara katika wilaya ya Kigamboni Waziri Bashungwa ameeleza kwamba, serikali ya awamu sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeridhia ujenzi wa barabara ya kutoka Kibada kwenda Mwasonga hadi Kimbiji yenye urefu wa kilometa 41.

Licha ya uharibifu unaotokea Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kupitia kitengo cha dharura imekuwa ikirudisha mawasiliano kwenye maeneo ambayo mawasiliano yamekatika kutokana na uharibifu.

Kwa upande mwingine, Waziri Bashungwa ameagiza kuundwa kwa timu maalumu na kisha kupelekwa katika eneo la Magogoni lililopo kata ya Tungi wilayani Kigamboni kwa ajili ya kufanya usanifu na kisha kuja na majawabu ya juu ya nini kifanyike ili kutatua changamoto ya maji kuzingira makazi ya wananchi wa eneo hilo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema mkoa huo unahitajika kufumuliwa kwenye mifumo imara na thabiti ya kusafirisha maji ya mvua lengo likiwa ni kuondoa athari zinazotokana na mafuriko ikiwemo wananchi kupoteza maisha.