Back to top

BASHUNGWA AKAGUA UJENZI HOSPITALI YA WILAYA KIBAHA, BIL 3.5 ZATUMIKA

09 October 2024
Share

Waziri wa Ujenzi, Mhe.Innocent Bashungwa, amekagua ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha na kuridhishwa na matumizi ya fedha kwa awamu yaliyotolewa na Serikali ambapo kiasi cha shilingi Bilioni 3.5, kimetumika katika ujenzi wa majengo mbalimbali katika Hospitali hiyo.

Bashungwa amekagua ujenzi huo Mkoani Pwani, akiwa katika ziara yake maalum ya kukagua utekelezaji wa miradi, kuzindua miradi ya maendeleo pamoja na kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi katika Mkoa huo.

Bashungwa amemshukuru na kumpongeza Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha za kuimarisha huduma za afya nchini.

"Nimshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amewajali na kuhakikisha fedha hizi zinapatikana katika ujenzi wa hospitali hii" Amesema Bashungwa.

Bashungwa ameutaka Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kuhakikisha thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali katika hospitali hiyo inaonekana kwa kukamilisha ujenzi  lna kutunza majengo mengine yaliyokamilka.

Aidha, Bashungwa ameutaka Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha na Hospitali hiyo kuhakikisha wanatunza mazingira kwa kupanda miti ya vivui na matunda katika eneo lq Hospitali hiyo.

Kadhalika, Bashungwa ameeleza kuwa Serikali ipo katika hatua ya manunuzi ya kumpata Mkandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara ya Mlandizi - Ruvu (km 23) kwa kiwango cha lami ili kuunganisha barabara hiyo pamoja na Stesheni ya Reli ya Kisasa ya SGR ya Ruvu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, ameeleza kuwa hadi sasa Mkoa huo una hospitali za Wilaya 10, Hospitali ya Rufaa 1, Vituo vya Afya 50, Zahanati 388, sehemu za kujifungulia (maternity wards) 22 na hivi karibuni watapata Hospitali nyingine kubwa Rufiji kutokana CSR ya mradi wa Bwawa la Nyerere 

Naye, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dkt. Christopher Ngendelo ameeleza kuwa Hospitali ya Wilaya ya Halmashauri ya Kibaha ilianza kutoa huduma mwaka 2020 na hadi sasa ina jumla ya majengo 15 yakiwemo Jengo la wagonjwa wa nje, jengo la maabara, jengo la mionzi, wodi ya wazazi cha upasuaji wa dharura na chumba, jengo la utawala, jengo la ufuaji, jengo la wodi ya watoto, jengo la upasuaji, jengo la kuhifadhia maiti, jengo la kuchomea taka, jengo la upasuaji la wanaume na wanawake pamoja na jengo la stoo.