Back to top

BASHUNGWA:TRA SIMAMIENI MIONGOZO NA KAULI WEZESHI KWA WAFANYABIASHARA

27 March 2024
Share

Waziri wa Ujenzi ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Karagwe Mh. Innocent Bashungwa ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoa wa Kagera kusimamia miongozo pamoja na kutoa elimu ya Sheria na Kanuni za kodi mara kwa mara kwa wafanyabiashara pamoja na Maafisa kuwa na kauli nzuri na wezeshi.

Bashungwa amezungumza katika kikao kilichowakutanisha wafanyabiashara wa Wilaya ya Karagwe pamoja na Taasisi za Serikali zinazowahudumia ambapo amesikiliza kero zao ikiwemo tozo kubwa za kodi, ushuru pamoja na kauli zisizoridhisha kutoka kwa Maafisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA).

Bashungwa amesisitiza kuwa ukusanyaji wa mapato unawezesha Serikali kufanikisha malengo yake ya kuhudumia nchi pamoja na wananchi wake kwa haraka kwa kuwa wajibu wa Serikali ni kujenga ustawi wa wafanyabiashara na sio kuwadumaza.

“Sijafurahishwa na madai ya kauli za Maafisa kwa wafanyabiashara ambazo sio sahihi,kwa  kuwaaambia wakishindwa kulipa kodi,  wafunge biashara, Lengo la Serikali ni kuwawezesha kwa kutoa elimu, kuwashauri na kustawisha wafanyabiashara” amesisitiza Bashungwa.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Kagera, Bw. Omary Kigoda amesema kuwa suala la lugha mbaya kwa walipa kodi sio msimamo wa Taasisi hivyo TRA itaendelea kuwachukulia hatua baadhi ya watumishi ambao wanaenda kinyume na maadili ya utumishi.

Bashungwa amelitaka Baraza la wafanyabiashara la Wilaya ya Karagwe kutimiza wajibu wao kwa kuitisha mikutano ya mara kwa mara na wafanyabiashara wote ili kukumbushana masuala tozo mbalimbali zilizopo na kutatua changamoto zao kwa kuzipatia suluhu ya haraka kabla mfanyabiashara hajafikia hatua ya kufunga biashara.