Serikali imesaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya Iringa - Msembe, inayoelekea kwenye Hifadhi ya Taifa ya Ruaha (km 104) kwa kiwango cha lami, utakaogharimu shilingi Bilioni 142.56 ili kufungua fursa za kiutalii, kiuchumi na kibiashara kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
Utiaji saini mikataba miwili kati ya Wakala ya Barabara (TANROADS), na Mkandarasi wa Ujenzi pamoja na Mhandisi Mshauri umefanyika Septemba 21, 2024, katika Uwanja wa Samora Mkoani Iringa.
Akizungumza na wananchi, Waziri wa Ujenzi, Mh. Innocent Bashungwa, amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara (TANROADS), kuhakikisha anamsimamia Mkandarasi wa kampuni ya CHICO aliyeshinda zabuni, kutekeleza ujenzi wa barabara hiyo kwa ubora na viwango, na kukamilisha kazi ndani ya muda kwa mujibu wa mkataba.
Vilevile, Bashungwa amesema kuwa, serikali inaendelea na jitihada mbalimbali za kuunganisha Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa barabara za lami ili kuboresha miundombinu ya usafiri, kurahisisha biashara, na kukuza uchumi.
Kwa upande wake Waziri wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Bunge, Sera na Uratibu William Lukuvi, ameeleza kuwa ujenzi wa barabara ya Iringa - Msembe ukikamilika kwa kiwango cha lami utafungua uchumi wa wananchi wa Iringa kwa kuwa tayari Serikali imekamilisha ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Nduli na hivyo wananchi watashuhudia makampuni mengi ya kitalii yakiongezeka.