Back to top

BOSI MPYA KARIAKOO ATAKA MABADILIKO

04 April 2025
Share

Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko Kariakoo, CPA Ashiraph Yusufu Abdulkarim, amewataka watumishi wa shirika hilo kuhakikisha wanafanya mageuzi katika utendaji kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu, Miongozo pamoja na taaluma zao ili kuleta matokeo chanya katika Shirika hilo.
 
CPA Ashiraph ametoa wito huo Jijini Dar Es Salaam, katika hafla fupi ya kukabidhiwa Ofisi na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu Bi. Mary Maridadi.
 
CPA Abdulkarim mesema kuwa kila mtumishi anawajibika kusimama katika nafasi yake na kufanya kazi kwa bidi ili kufikia malengo ya Shirika hilo. 
 
“Mtazamo wangu ni kwamba endapo watumishi watafanya kazi kila mmoja katika sehemu lake ni dhahiri kwamba uzalishaji utaongezeka na mazingira ya kazi yataboreshwa na kuleta ufanisi mzuri katika utendaji kazi wetu” ameeleza CPA Abdulkarim.

Vile vile CPA Abdulkarim amesisitiza nidhamu na uadilifu mahali pa kazi kuwa ni  suala muhimu sana ambapo vikikaa sawa uleta matokeo chanya, kwani watumishi wanapokosa nidhamu na uadilifu wanaharibu taswira ya Shirika na hawawezi kutumia muda wao vizuri katika kutekeleza majukumu kikamilifu.
 
“ Hivyo ni vema kila mmoja ajenge tabia ya kuwa muadilifu na mwenye nidhamu thabiti itakayomfanya kuepuka vitendo visivyofaa, kutumia muda wake vizuri, kuwahi kazini, na kutekeleza majukumu kwa mujibu wa miongozo na hatimaye kuwa na mchango chanya katika Shirika’,  ameongeza CPA Abdulkarim.
 
Aidha, napenda kuwashukuru Mwenyekiti wa Bodi, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Menejimenti ya Shirika na Watumishi wote kwa kazi nzuri mnayofanya na pongezi zenu na ushiriki wenu katika kikao hiki kifupi cha ukaribisho na makabidhiano ya Ofisi.
 
Amesema kuwa ana imani na watumishi wa shirika hilo katika kushirikiana kwa namna inayofaa katika kulifanya Shirika lisonge mbele na kujiendesha kwa tija.
 
Amesema matarajio yake ni kwamba watafanya kazi kuhakikisha kwamba hakuna uvujaji wa mapato, vyanzo vya mapato vinaongezeka, matumizi yanabanwa na Mipango ya kibiashara inawekwa thabiti huku mazingira ya kazi yanaboreshwa.
 
Amesisitiza kuwa jambo la muhimu ni kila mmoja kusimama katika nafasi yake na kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kwa kasi inayohitajika ili kuleta ufanisi katika utendaji kazi.
 
Aidha amemshukuru Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumuaniamini na kumteua katika nafasi hiyo na kuwapongeza Bodi ya wadhamini ikiongozwa na Mwenyekiti wake, watumishi wote kwa kazi nzuri waliyofanya na kwa mapokezi mazuri.