
Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, amesema kukamilika kwa Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Maji Kidunda, kutaongeza uhakika wa upatikanaji wa huduma ya majisafi na Salama kwa wakazi wa Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Morogoro.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameelekeza kuwa ni lazima mradi huo uwanufaishe majirani wote wanaozunguka mradi huo, ikiwemo Tarafa nzima ya Ngerengere na vijiji vyake.
Akizungumza na wakazi wa Kidunda Mkoani Morogoro, mara baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye Bwawa hilo, linalojengwa na Serikali ya Tanzania kwa gharama ya shilingi bilioni 335, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa bwawa la Kidunda linatarajiwa kutoa manufaa mengi, ikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama ya kunywa, uzalishaji wa umeme, kuendeleza shughuli za uvuvi, na kuimarisha barabara ya Kidunda kutoka Ngerengere.
Waziri Mkuu amekumbusha kuhusu umuhimu wa utunzaji wa vyanzo vya maji, akisisitiza kuwa ajenda ya utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji ni jukumu la kila Mtanzania. "Kuna umuhimu mkubwa wa kuhakikisha kwamba tunahifadhi na kuvitunza vyanzo hivi vya maji vinavyoleta maji mto Ruvu ili kuhakikisha kuwa bwawa hili linakuwa na ukubwa utakaojaza maji lita bilioni 190.
Kwa upande wake Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, amesisitiza kuwa wananchi ambao hawajalipwa fidia kutokana na utekelezaji wa mradi huo watalipwa stahiki zao, kuhakikisha kuwa haki za wananchi zinazohusiana na mradi huu zinazingatiwa.
Aidha Mradi wa Bwawa la Maji Kidunda ambao umefikia asilimia 28, unatarajiwa kuboresha maisha ya wakazi wa maeneo husika kwa kutoa maji ya uhakika, nishati ya umeme, na fursa nyingine za kiuchumi, kwa kuzingatia kuwa ni mradi wa kimkakati kwa maendeleo ya taifa.