Back to top

DHAMIRA YA RAIS WANANCHI WANUFAIKE NA MIRADI YA MAENDELEO

09 September 2024
Share

Naibu Waziri Nishati, Mhe.  Judith Kapinga amesema kuwa dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha wananchi wananufaika na miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao.

Kapinga amesema hayo wilayani Mtwara, mkoani wa Mtwara, wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, iliyolenga kukagua visima vya kuzalisha Gesi Asilia, katika eneo la Mnazi Bay pamoja na miradi inayofanyika kwa manufaa ya jamii kutokana na uwepo wa gesi hiyo  (CSR), ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Afya  na Kituo cha Polisi katika eneo la Msimbati.

"Yote haya mnayoyaona ni matunda ya kazi nzuri ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anaonesha kwa vitendo jinsi anavyowajali kwa kuhakikikisha mnapata huduma bora kupitia miradi hii." Amesisitiza Kapinga

Ameeleza kuwa lengo la ziara hiyo ya Kamati ya Bunge ni kujionea  thamani ya miradi hiyo ambayo itanufaisha wananchi wa Msimbati, ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Naibu waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,  Mhe. Dkt. Doto Biteko aliyoyatoa Novemba 15, 2024 mara baada ya kutembelea eneo hilo na kuzungumza na wananchi.

Amesema ujenzi wa kituo cha Afya unatarajiwa kukamilika  tarehe 30 Septemba, 2024 huku ujenzi wa Kituo cha Polisi nao ukiwa ukingoni.

Kapinga amesisitiza kuwa,  Serikali ipo pamoja na wananchi katika kuhakikisha inawapelekea maendeleo.

Katika hatua nyingine,  Kapinga amewaasa wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa kwa kuanza kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.