Back to top

DKT. BITEKO AWAASA WAISLAMU KUENDELEA KUHIFADHI QURAN TUKUFU

09 February 2025
Share

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewaasa waislamu nchini kuendelea kumcha Mungu na kutenga muda wa kujifunza na kuisoma Qur’aan Tukufu ambayo itawafunza mambo mema yaliyoelekezwa na Mwenyezi Mungu.

Dkt. Biteko amesema hayo, jijini Dar es Salaam wakati akizindua  Mashindano Makubwa zaidi ya Qur’aan Tukufu Ulimwenguni 2025.

“ Nawaomba msivunjike moyo akitokea mwenye tafsiri tofauti nyie msivunjike moyo wala kukatishwa tamaa bali mfanye mashindano haya yawe kinara na kuutangaza uislamu katika ulimwengu,” amesema Dkt. Biteko.

Pia amewahimiza kumuomba Mungu ili Qur’aan iwanyanyue na isiwabwage katika shughuli mbalimbali wanazofanya kama kaulimbiu ya mwaka huu inavyosema “ Qur’aan Ikunyanyue, Isikubwage”.

Amesema Qur'aan inatoa funzo kwa watu na kuwa  waasisi wake  waliyaanzisha kwa ngazi ya madrasa lakini baadaye kutokana na umuhimu wake yakavutia wengi zaidi na kuwa mashindano ngazi ya mtaa, kata, wilaya, mkoa hadi kuwa  ya Afrika Mashariki, Bara la Afrika na kisha kufikia ngazi ya kuwa mashindano ya Ulimwengu

“ Mashindano haya mbali na kuwa yanachochea usomaji wa Qur’aan Tukufu na hivyo kujenga uelewa wa hofu ya Mwenyezi Mungu lakini pia yanaitangaza Tanzania katika taswira chanya,” amebainisha Dkt. Biteko.

Ameendelea kusema kuwa Nabii Musa aliwalingania watu wake kwa kutumia muongozo kutoka katika Taurati, Nabii Daudi yeye akatumia Zaburi, Nabii Issa (Yesu) akatumia Injili na Mtume Muhamad swalla llahu alayhi wasallam akatumia Qur’aan tukufu kuwalingania watu wa umma wake. 

"Kimsingi vitabu hivi vya muongozo vinamfundisha binadamu tabia njema na kumsihi kuzishikilia na kumuonesha tabia zisizofaa na kumuasa kukaa mbali nazo.”

Dkt. Biteko amerejea aya katika Qur’aan tukufu sura ya 35, Surat Faatir, aya ya 28 “… kwa hakika wanaomcha Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wanazuoni”.  

Amefafanua “ Aya hii ina maanisha kuwa wale waliopata ujuzi na mafundisho ya Mwenyezi Mungu ambayo yanapatikana katika Qur’aan tukufu na kuyazingatia yale waliyojifunza ndio wanaofika daraja la uchamungu.”

Vilevile, Dkt. Biteko ameipongeza Taasisi ya Al- Hikma kwa jitihada zake za kukuza Mashindano ya kuhifadhi Qur’aan Tukufu ulimwenguni.

Mkurugenzi Mkuu wa Al- Hikma na Mwenyekiti wa Mashindano ya Qur’aan Tukufu Ulimwenguni, Sheikh  Nurdin Kishk amesema kuwa mashindano hayo yameendelea  kukua kila mwaka kutokana na mapenzi ya kuhifadhi Qur’aan.

Aidha, ameishukuru Serikali kwa ushirikiano wake na kwa kuridhia mashindano hayo kufanyika katika Uwanja wa Taifa mnamo Machi 16, 2025 ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.