
Baraza la mawaziri la Kamisheni ya Pamoja ya Bonde la Mto Songwe limemteua Dkt. Mhandisi Ladislaus Kyaruzi Leonidas kuwa Katibu Mtendaji wa kwanza wa Kamisheni ya Pamoja ya Bonde la Mto Songwe (SONGWECOM).
Kamisheni ya Pamoja ya Bonde la Mto Songwe inaundwa kwa pamoja na nchi za Tanzania na Malawi ambapo mwaka 2019 Tanzania na Malawi zilizindua Kamisheni hii kwa lengo la kuendesha miradi ya umwagiliaji na uzalishaji wa umeme kutoka nishati jadidifu yenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 860.
Dkt Kyaruzi ambaye ni Mhandisi na mwenye Shahada ya Uzamivu katika Mabadiliko ya Tabianchi na Maendeleo Endelevu ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) anaanza majukumu yake tangu Julai, 2023, baada ya kuchukua nafasi ya Bw. Hyde R.G. Sibande aliyekuwa akikaimu nafasi ya Katibu Mtendaji wa Kamisheni hiyo.
Kabla ya uteuzi wake mpya, Dkt Kyaruzi alikuwa Mkuu wa Idara ya Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) anayehusika na mazingira na maliasili.
Mwaka 2011-2021, alihudumu katika majadiliano ya kikundi cha Kiafrika kinachojadiliana juu ya mabadiliko ya tabianchi kwa mchakato wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tanianchi wa Umoja wa Mataifa .
Dkt Kyaruzi pia ni mjumbe wa Kamati Tendaji ya Teknolojia ya Kimataifa kwenye Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (2018 hadi sasa).
Dkt Kyaruzi pia amesimamia marekebisho ya Itifaki ya usimamizi wa mazingira na maliasili katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Pia aliratibu uendelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa mabadiliko ya tabianchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa upande wa uongozi na uhusiano na mashirika au taasisi zinazofanana za kikanda na kimataifa, kuanzia 2016-2017, Dkt Kyaruzi alikuwa Mwenyekiti wa tawi la uwezeshaji Duniani la Kamati ya ufuatiliaji ya Itifaki ya Kyoto kwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (Global Facilitative Branch of the Compliance Committee of the Kyoto Protocol to the United Nations Framework Convention on Climate Change).
Lakini pia Dkt Kyaruzi aliwahi kuwa Makamu mwenyekiti wa tawi la uwezeshaji duniani la kamati ya ufuatiliaji ya Itifaki ya Kyoto tangu 2014 hadi 2015.
Vilevile kwa mwaka 2013-2014 alikuwa Mjumbe wa timu ya wataalamu kutoka Tanzania kwa Mratibu wa Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali za Afrika kuhusu Mabadiliko ya tabianchi (the Coordinator of the Committee of African Heads of State and Government on Climate Change (CAHOSCC)) wakati Tanzania iliporatibu CAHOSCC.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji , Mheshimiwa Jumaa Aweso (Mb) amempongeza Dkt Kyaruzi kwa kuteuliwa na kuongeza kuwa ana imani kuwa, Kamisheni ya Pamoja ya Bonde la Mto Songwe iko katika mikono salama.