Back to top

Erick Kabendera kuendelea kusota rumamande, upelelezi haujakamilika.

19 August 2019
Share

Tayari akiwa amekwisha kaa mahabusu kwa tarbani wiki mbili, upelelezi wa kesi ya kuongoza genge la Uhalifu na utakatishaji fedha wa zaidi ya Sh.Milioni 100 inayomkabili Mwandishi Wa Habari za uchunguzi Erick Kabendere haujakamilika

Kabendera amerudishwa tena mahakamani leo ambapo kwa ajili ya shauri lake kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Augustine Rwizile.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amemueleza Hakimu Mkazi, Agustina Mmbando kuwa shauri hilo limeitishwa kwa ajili ya kutajwa na ilitakiwa kutajwa mbele ya Hakimu Rwezile lakini hayupo.

Wakili Wankyo amedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo anaomba iahirishwe hadi tarehe nyingine.

Wakili wa Kabendera, Jebrah Kambole amedai kuwa hawana pingamizi isipokuwa mshitakiwa yupo gerezani na kesi yake haina dhamana hivyo waharakishe suala la upelelezi.

Baada ya kueleza hayo, kesi hiyo imeahirishwa hadi August 30, 2019 kwa ajili ya kutajwa.

Miongoni mwa mashitaka yanayomkabili Kabendera anadaiwa katika siku tofauti tofauti kati ya Januari 2015 na Julai 2019 katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam, alitoa msaada katika genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia faida.

Pia anadaiwa bila kuwa na sababu za msingi kisheria alishindwa kulipa kodi ya sh. 173, 247,047.02 ambayo ilitakiwa ilipwe kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)

Aidha anadaiwa mshtakiwa alijipatia kiasi hicho cha sh. Milioni 173.2 wakati akizipokea alijua kuwa fedha hizo ni mazao ya makosa tangulizi ya kukwepa Kodi na kujihusisha na genge la uhalifu.