Wizara ya Katiba na Sheria imeendesha mafunzo ya utawala bora yaliyofanyika mkoani Iringa, zikihusisha Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo na Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Mkuu wa Wilaya ya Iringa Bw.Herry James aliwashukuru waandaaji na washiriki wa mafunzo haya kwa kujitokeza kwa wingi ambapo amesisitiza umuhimu wa mafunzo haya katika kuongeza uelewa wa masuala ya Demokrasia, Haki za Binadamu, Utawala bora, na majukumu ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama.
“Lengo kuu la mafunzo haya ni kuwajengea uwezo viongozi katika ngazi mbalimbali za utawala ili kuhakikisha tunazingatia misingi ya utawala bora, haki za binadamu, na demokrasia kwa vitendo,” alisema Bw. Herry James, Mkuu wa Wilaya ya Iringa.
Bw. Herry alibainisha kuwa mafunzo haya yanahusisha wajumbe wa Kamati za Usalama za Mkoa na Wilaya, baadhi ya wataalam wa Halmashauri, na Watendaji wa Kata zote za Mkoa wa Iringa. Pia alieleza kuwa mafunzo ya ngazi ya Halmashauri yatafanyika kwa Kamati za Usalama za Wilaya, wataalam, na watendaji wa kata.
Kwa upande wake Mratibu wa Mafunzo kutoka Idara ya Katiba na Ufuatiliaji Haki Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Dorice Dario, Wakili wa Serikali Mkuu daraja la kwanza amesema kuwa Wizara imeanza mchakato wa kuhakikisha elimu hii inayafikia makundi mbalimbali ili kujenga uelewa wa pamoja na kuwajengea Uzalendo makundi mbalimbali ya Watendaji
Baadhi ya changamoto zinazokabili Mkoa wa Iringa ni pamoja na uelewa mdogo wa masuala ya Haki za binadamu, mila na desturi kandamizi, vitendo vya ukatili wa kijinsia, pamoja na imani za kishirikina. Alitoa wito kwa washiriki wa mafunzo hayo kushirikiana kutatua changamoto hizi kwa kushirikisha maarifa watakayopata.