Back to top

HOSPITALI YA RUFAA BOMBO TANGA KUWA NA MUONEKANO MPYA

22 February 2025
Share

Serikali kupitia Wizara ya Afya imejipanga kuanza ujenzi na ukarabati wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga (Bombo) kwa kuanzia na jengo la wodi ya mama na mtoto kabla ya mwezi Mei mwaka huu, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za uzazi mama na mtoto na kuwa katika muonekano mpya. 

Kauli hiyo imetolewa na Mhe. Jenista Mhagama leo Februari 22, 2025 alipofanya ziara katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Tanga (Bombo) ambapo ametumia fursa hiyo kuihamasisha jamii ya mkoa huo kujitokeza kumpokea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa ziara yake mkoani humo. 

"Serikali ya awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imeipa kipaumbele Sekta ya Afya ambapo zaidi ya Shilingi Trilioni 8 zimewekezwa kwa kipindi hiki kifupi, ukiwemo mkoa wa Tanga," amesema Waziri Mhagama.

Amesema kwa sasa Serikali inafanyia kazi changamoto ya majengo katika hospitali ya Bombo ambapo kwa ujenzi utaanza kwa kubadilisha muonekano wa hospitali hiyo na kuanza na jengo ya wodi wazazi ambalo litakuwa na huduma zote fungamanishi ikiwemo upasuaji pamoja na vipimo vya maabara. 

"Kiu ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona  tunaendelea kupunguza vifo vya mama na mtoto, kutoka  vifo 556 kwa vizazi hai 100,000 hadi vifo 104 kwa vizazi hai 100,000, pia tungetamani hospitali yetu ya Bombo iendelee kuongoza kwenye zoezi la kuondoa vifo vya kina mama wakati wa kujifungua," amesema Waziri Mhagama.

Waziri Mhagama ametumia wasaa huo kuihamasisha jamii ya watu wa mkoa wa Tanga kujitokeza kwa wingi kumpokea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwakuwa ameonesha uwezo wa kusimamia miundombinu ya utoaji wa huduma za afya.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa mkoa wa Tanga (Bombo) Dkt. Frank Shega ameomba kuwezeshwa kifedha ili kukarabati  majengo ya hospitali hiyo pamoja na  kujenga majengo mengine mapya kwa ajili ya kuongeza huduma na kuwa na uwezo mkubwa wa kutoa huduma za afya kwa wananchi.