Back to top

HUDUMA YA M-MAMA YAWASADIA WANAWAKE 3,430 ARUSHA

07 March 2025
Share

Huduma ya M-Mama ni mojawapo ya miradi muhimu ya afya iliyoanzishwa na Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kusaidia kina mama wajawazito na watoto wachanga kupata huduma bora za afya, ambapo Huduma hii inatumia teknolojia ya simu kuunganisha wajawazito na huduma za dharura za usafiri, kuhakikisha wanapata matibabu kwa haraka wanapohitaji msaada wa kiafya.

Katika Mkoa wa Arusha, huduma ya M-MAMA imewanufaisha wanawake 3,430, moja ya faida kubwa za huduma ya M-Mama ni kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga kwa kuhakikisha wagonjwa wanawasiliana haraka na hospitali au zahanati kwa ajili ya usafiri wa dharura. 

Huduma hii inawasaidia wanawake, hasa wale wa maeneo ya Vijijini, ambako huduma za afya zinaweza kuwa mbali au usafiri wa kawaida ni mgumu, Pia imeboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wakati, kwani kina mama Arusha wanapata msaada mara moja kupitia mfumo huu.

Huduma ya M-Mama imepunguza gharama za usafiri kwa kina mama wajawazito, wengi wao walikuwa wakikumbwa na changamoto za kifedha wakati wa kusafiri kwenda hospitali kwa ajili ya kujifungua. Huduma hii inahakikisha kwamba usafiri wa dharura unapatikana bila gharama kubwa, hivyo kusaidia wanawake wa kipato cha chini.

Aidha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi siku ya kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, ambayo inaadhimishwa Machi 08, 2025 katika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.